Swali: Muulizaji anauliza juu ya kutawadha kwa ajili ya kusoma Qur-aan?

Jibu: Qur-aan tukufu ni maneno ya Allaah, Kitabu kitukufu zaidi na ndio Kitabu cha mwisho kilichoteremshwa kutoka mbinguni. Miongoni mwa uadhimisho wa Allaah juu yake amesema (Subhaanah) juu yake:

إِنَّهُ لَقُرْآنٌ كَرِيمٌ فِي كِتَابٍ مَّكْنُونٍ لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ

“Hakika hii ni Qur-aan tukufu. Katika Kitabu kilichohifadhiwa. Haigusi isipokuwa waliotakaswa kabisa.”[1]

Pia imepokelewa katika Hadiyth ya kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaandikia watu wa Yemen:

“Asiiguse Qur-aan isipokuwa aliye na twahara.”

Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walifutu hivo. Kwa ajili hiyo kikosi cha wanazuoni wengi – wakiwemo wale maimamu wanne – wameona kuwa haijuzu kuigusa Qur-aan isipokuwa kwa aliye msafi kutokamana na hadathi mbili; ndogo na kubwa. Ni kama ambavo haijuzu kwa hali zote kwa mwenye janaba kuisoma isipokuwa mpaka aoge kutokamana na janaba, na maoni haya ndio ya sawa.

Haifai kwa mwenye hadathi kusoma Qur-aan ndani ya msahafu. Lakini hata hivyo inafa kwake kusoma kwa hifdhi ya moyo ikiwa hadathi yake ni ndogo. Kuhusu mwenye janaba haifai kwake kuisoma kwa hali zote mpaka aoge kwanza. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuna kitu kilichokuwa kinamzuilia kutokamana na [kuisoma] Qur-aan isipokuwa anapokuwa na janaba. Hayo yamethibiti kutoka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Hakuna kitu kilichokuwa kinamzuilia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokamana na Qur-aan isipokuwa janaba peke yake.”

Wanazuoni wametofautiana juu ya mwenye hedhi na mwenye damu ya uzazi kama wana hukumu moja kama ya mwenye janaba? Baadhi yao – na ndio wengi – wameona kuwa ana hukumu moja kama ya mwenye janaba. Wamemzuilia kusoma Qur-aan kwa hali zote mpaka kwanza asafike. Kumepokelewa Hadiyth juu ya jambo hilo aliyopokelewa na Abu Daawuud kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hasomi mwenye hedhi wala mwenye janaba chochote katika Qur-aan.”

Wengine wakasema kuwa inafaa kwake kusoma kwa hifdhi ya moyo. Vinginevyo muda utawarefukia na jambo haliko mikononi mwao kama mwenye janaba. Haya ndio maoni ya sawa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha ´Aaishah katika hajj ya kuaga hali ya kuwa ni mwenye hedhi: afanye yale yote anayofanya mwenye kuhiji mbali na kutufu. Hakumkataza na kusoma Qur-aan. Kumlinganisha mwenye hedhi na nifasi juu ya mwenye janaba si sahihi kutokana na ukubwa wa kutofauti kati ya wawili hao na mtu huyo.

Hadiyth ya Ibn ´Umar iliyotajwa ni dhaifu kwa mtazamo wa wanazuoni. Ni miongoni mwa mapokezi ya Ismaa´iyl bin ´Ayyaash, kutoka kwa Muusa bin ´Aqabah. Bwana huyu ni kutokea Hijaaz. Mapokezi ya Ismaa´iyl anapopokea kutoka kwa wengine – mbali na watu wa Shaam – mapokezi yake huhesabika ni dhaifu.

[1] 56:77-79

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/146)
  • Imechapishwa: 24/08/2021