Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Waumini watamuona Mola Wao Aakhirah kwa macho yao. Watamtembelea; Ataongea nao na wao wataongea Naye. Anasema Allaah (Ta´ala):

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.” (75:22-23)

Vilevile akasema (Ta´ala):

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ

“Hapana! Hakika wao [makafiri] siku hiyo watawekewa kizuizi [wasimuone] Mola wao.” (83: 15)

Wakati Atawazuia watu hao katika hali ya Kutoridhika nao, ni dalili ioneshayo ya kwamba waumini watamuona katika hali ya Yeye Kuridhika. Vinginevyo kusingelikuwa baina yazo tofauti. Kasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kwa hakika nyinyi mtamuona Mola Wenu kama mnavyoona mwezi huu – hamtosongamana (kupata shida yoyote) katika Kumuona.” Hadiyth Swahiyh. Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ushabihisho huu ni ushabihisho wa maono, na si kwa kitachoonywa, kwa hakika Allaah (Ta´ala) hana anachofanana nacho wala anayelingana Naye.”

Miongoni mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunanh wal-Jamaa´ah ambayo wametofautiana kwayo na ´Aqiydah za wazushi ni kwamba wanaamini kuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) ataonekana siku ya Qiyaamah. Vilevile wanaamini kuwa haiwezekani kwa yeyote kumuona hapa duniani. Alisema (Jalla wa ´Alaa) kumwambia Muusa baada ya kumuomba kumuona:

لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِيۚ

“(Lan) hutoniona! Lakini tazama jabali. Likitulia mahali pake, basi utaniona.” (07:143)

Kumuona Allaah hapa duniani haiwezekani. Kuhusiana na Aakhirah ni jambo lenye kuwezekana, bali uhakika wa mambo ni kwamba itakuwa hivyo kama alivyoelezea Allaah (Jalla wa ´Alaa) pale aliposema:

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.” (75:22-23)

Waumini watamuona Mola Wao (Jalla wa ´Alaa) katika uwanja wa Qiyaamah na Peponi. Wataburudika kwa kule kuutazama uso wa Allaah mkarimu. Hakuna neema kubwa watayopewa kama kumuona Mola (Jalla wa ´Alaa). Hii ndio neema kubwa kabisa. Ndio maana Allaah (Jalla wa ´Alaa) akaita kuwa ni nyongeza pale aliposema:

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

“Kwa wale waliofanya mazuri watapata Pepo na zaidi.” (10:26)

Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Ziadi” ni kutazama uso wa Allaah (Ta´ala).””

Hadiyth hii ameipokea Muslim na wengineo.

Watu wa Bid´ah wamepinga hilo. Kuna pote lililosema asli ni kuwa Allaah hawezi kuonekana na vilevile asli ni kwamba Allaah kuonekana haikutokea si duniani wala Aakhirah. Haya ni maneno ya Jahmiyyah, Mu´tazilah na vifaranga vyao. Wanafasiri maneno Yake (Ta´ala):

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.”

na kusema kwamba kutazama (Naadhwirah) maana yake ni kusubiri. Wanasema ni kama mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا سُنَّتَ الْأَوَّلِينَ

“Je, basi wanangojea (Yandhwuruuna) nini isipokuwa desturi ya watu wa awali.” (35:43)

Bi maana wanasubiri. Kwa hivyo neno kutazama lililokuja katika Aayah ifuatayo:

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.”

wanasema kwamba maana yake ni kusubiri. Bi maana wanasubiri rehema na maamrisho ya Allaah. Vilevile wanatumia hoja hii Khawaarij wa sasa ambao ikiwa ni pamoja vilevile na Ibaadhiyyah na wenye kufuata madhehebu ya Mu´tazilah.

Mosi: Tunajibu hili kwa kusema maneno haya hata kilugha hayajanyooka, sembuse kabla hatujasema kwamba waumini kumuona Mola Wao (Jalla wa ´Alaa) ni jambo limethibiti katika dalili nyingi. Lakini tunapozungumzia kuhusiana na lugha ni kosa. Hilo ni kwa sababu Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“(Ilaa Rabbihaa Naadhwiyrah) Zikimtazama Mola wake.”

Tamko an-Nadhwar ni sahihi kwamba linaweza kuja kwa maana ya ´kusubiri`. Lakini hata hivyo linapokuja kwa maana ya ´kusubiri` mbele yake hapawepo ´ilaa`. Kwa mfano maneno Yake (Jalla wa ´Alaa):

فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً

“Je, basi wanangojea (Yandhwuruuna) nini isipokuwa Saa iwafikie ghafla?” (47:18)

فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا سُنَّتَ الْأَوَّلِينَ

“Je, basi wanangojea (Yandhwuruuna) nini isipokuwa desturi ya watu wa awali.” (35:43)

Pale ilipokuwa mbele yake hakukuwekwa neno “ilaa” basi hilo likatujuza kwamba an-Nadhwar iliokuja hapa maana yake ni kusubiri.

Ama neno an-Nadhwar likifuatana na herufi ´ilaa` maana yake ni kutazama kwa macho na si nyengine. Hakuna maana nyingine zaidi ya hii kwa mujibu wa lugha. Mfano wa hilo ni pale aliposema (Jall wa ´Alaa):

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. (Ilaa) Zikimtazama Mola wake.”

Pili: Dalili ya pili ni kwamba amesema (Jalla wa ´Alaa):

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.”

Ni kitu gani kinachomtazama Mola? Ni nyuso. Hii ni dalili kwamba maono haya ni kupitia macho. Kwa sababu (Jalla wa ´Alaa) amefanya kinachotazama ni nyuso. Kwenye uso ndio maeneo ya kuonea. Hizi dalili zinakanusha tafsiri ya an-Nadhawr kwamba ni kusubiri.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalish-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 90-92
  • Imechapishwa: 27/08/2020