Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

108 – Abu Swafwaan ´Abdullaah bin Busr al-Aslamiy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) amesema:

خَيرُ النَّاسِ مَنْ طَالَ عُمُرهُ، وَحَسُنَ عَمَلُهُ

“Mbora katika watu ni yule ambaye umri wake unakuwa mrefu na matendo yake yanakuwa mazuri.”

at-Tirmidhiy na amesema ni Hadiyth nzuri.

Katika Hadiyth hii kuna dalili juu ya kwamba kule umri wa mtu kuwa mrefu sio jambo lenye kheri kwa mwanadamu lenyewe kama lenyewe. Isipokuwa ikiwa kama atakuwa na umri mrefu na matendo yake yakawa mema. Kwa sababu wakati mwingine kurefuka kwa umri inakuwa ni jambo baya, lenye madhara na la shari kwa mwanadamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّمَا نُمْلِي لَهُمْ خَيْرٌ لِّأَنفُسِهِمْ ۚ إِنَّمَا نُمْلِي لَهُمْ لِيَزْدَادُوا إِثْمًا ۚ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ

“Na wala wasidhanie kabisa wale waliokufuru kwamba muhula tunaowapa [wa kustarehe] ni kheri kwao. Hakika tunawapa muhula ili wazidi [kufanya] dhambi – nao watapata adhabu ya kudhalilisha.” (03:178)

Makafiri hawa Allaah anawastarehesha kwa riziki, uzima, maisha marefu, watoto na wake, si kwamba ni jambo lenye kheri kwao. Uhakika wa mambo ni jambo lenye shari kwao. Kwa maisha marefu wanayopewa madhambi ndio yanazidi.

Kwa ajili hii ndio maana kuna wanachuoni ambao wamechukizwa kumuombea mwenzako kwa kusema “Allaah akupe maisha marefu.” Isipokuwa ikiwa kama utaomba hivo kwa kuambatanisha na  neno jingine “Allaah akupe maisha marefu kwa kumtii.” Kwa sababu maisha marefu ni jambo linaweza kuwa na shari kwa mtu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/107-108)
  • Imechapishwa: 27/02/2024