Watu aina mbili wanaoshuhudiliwa Pepo

Watu wa Peponi wamegawanyika sehemu mbili:

1 – Kundi la kwanza ni wale tunaoshuhudia kuwa wako Peponi kwa sifa zao.

2 – Kundi la pili ni wale tunaoshuhudia kuwa wako Peponi kwa dhati zao.

Ambao tunahushudia kuwa ni katika watu wa Peponi kutokana na sifa zao ni kila yule ambaye ni muunmini na mchaji Allaah. Watu wenye sifa hizi tunashuhudia kuwa ni katika watu wa Peponi. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema kuhusu Pepo:

أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ

“Imeandaliwa kwa wenye wenye kumcha Allaah.”  (03:133)

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ جَزَاؤُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا

“Hakika wale walioamini na wakatenda mema – hao ndio wema wa viumbe. Malipo yao yako kwa Mola wao, [nayo ni] mabustani za ‘Adn zipitazo chini yake mito ni wenye kudumu humo milele.” (98:07-08)

a) Kila ambaye ni muumini na anamcha Allaah na anafanya matendo mema, sisi tunashuhudia ya kwamba ni katika watu wa Peponi. Lakini hata hivyo hatusemi kuwa ni fulani bin fulani kwa sababu hatujui mwisho wake utakuwa vipi na hatujui kama undani wake ni kama uinje wake ulivo. Kwa ajili hiyo ndio maana hatuwezi kushuhudia kwa dhati yake. Anapokufa mtu na uinje wake unaonekana ni kheri tunachosema ni kwamba twataraji kuwa ni katika watu wa Peponi. Lakini hatuwezi kukata uamuzi wa moja kwa moja na kusema ni katika watu wa Peponi.

b) Kundi lingine tunashuhudia kwa dhati zao. Hawa ni wale ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameshuhudia na kusema kuwa ni katika watu wa Peponi. Kwa mfano wale Maswahabah kumi waliobashiriwa Pepo; Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy, Sa´iyd bin Zaydm Sa´d bin Abiy Waqqaas ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, Twalhah bin ´Ubaydillaah, Abu ´Ubaydah ´Aamir bin al-Jarraah, Zubayr bin ´Awwaam. Allaah awawie radhi wote.

Wengine ni Thaabit bin Qays bin Shammaas, Sa´d bin Mu´aadh, ´Abdullaah bin Salam, Bilaal bin Rabaah. Allaah awawie radhi wote. Hawa na wengineo ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewataja kwa dhati zao. Hawa tunashuhudia kwa dhati zao. Tunasema ya kwamba tunashuhudia kuwa Abu Bakr yuko Peponi, tunashuhudia kuwa ´Umar yuko Peponi, tunashuhudia kuwa ´Uthmaan yuko Peponi, tunashuhudia kuwa ´Aliy yuko Peponi na kadhalika.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/236)
  • Imechapishwa: 05/03/2023