Wajinga hawafahamu namna Mitume walivyolingania

Swali 37: Baadhi wanasema kuwa ulinganizi wa Salafiyyah ni wa kufuata mkombo na hauendani na zama hizi ambazo zimejaa fitina. Kwa hiyo mlinganizi anahitaji kutumia njia na mifumo mingine. Kama ambavyo madhambi yamekuwa aina mbalimbali ni lazima vilevile kuwepo njia mbalimbali za kulingania.

Jibu: Watu hawa ni masikini. Ugonjwa na matatizo yao ni kwamba hawajui namna ambavyo Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walivyolingania. Wanasahau ulinganizi wa Mitume pindi wanapopiga vita ulinganizi wa Salafiyyah na wanataka kuichafua. Je, matatizo haya na mitihani haikuwepo wakati wa Nuuh (´alayhis-Salaam)? Je, wakati wa Nuuh kulikuweko shirki peke yake? Vipengele vyengine vyote vya kimaisha vilikuwa salama? Hakukuwepo maasi wala ufisadi? Matatizo na kipingamizi chao maana yake ni kwamba ulinganizi wa Nuuh (´alayhis-Salaam) haukuwa wa sawa. Kwa sababu ulinganizi wake ulikuwa unazungumzia ´Aqiydah, unaofuata mkumbo na hautatui matatizo ya jamii.

Hebu tuseme kuwa tunapambana na matatizo yote yanayowasibu watu isipokuwa tu mambo yanayoiathiri Tawhiyd; ni kipi tumewafaa watu? Manufaa yako wapi ikiwa tutapambana na matatizo yote isipokuwa tu shirki?

Wanasema kuwa wanataka kuwafanya waislamu kuwa kitu kimoja. Wanasema kwamba kuna maasi na kwamba hakuna nchi ya Kiislamu. Wanasema kuwa wanataka kuanza na kitu hicho na wanapomaliza kazi hiyo ndipo wataanza na Tawhiyd? Wamemaliza kazi yao na bado hawajaanza na shirki na umoja wa dini, lakini bado wamesahau ulinganizi wa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam).

Ulinganizi wa Salafiyyah ndio ulinganizi sahihi katika hali zote. Ikiwa kuna shirki na Bid´ah basi wanapambana na shirki na Bid´ah kabla ya kupambana na maasi. Tunazungumzia pia maasi, lakini mkazo wetu unakuwa katika ile njia ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) katika kupambana na shirki. Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) wakati fulani walikuwa wanaweza kupuuza baadhi ya vitu, lakini jukumu kubwa ilikuwa kutokomeza shirki na kusimamisha Tawhiyd.

Ulinganizi wa Salafiyyah umejengeka juu ya elimu na juu ya njia ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Wanaipa kipaumbele Tawhiyd kabla ya kila kitu. Huyu ambaye anamwabudu Allaah pekee na ana madhambi mfano wa mlima atatoka Motoni ima kabla au baadaye. Lakini ni wapi ataingia mtu ambaye ana matendo mema mfano wa mlima lakini hata hivyo akawa hana Tawhiyd?

وَقَدِمْنَا إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاء مَّنثُورًا

”Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya matendo yoyote yale na Tutayafanya kuwa ni mavumbi yaliyotawanyika.”[1]

Kuhusu mpwekeshaji atarehemewa na Allaah licha ya kuwa ana madhambi mengi:

”Allaah (Ta´ala) amesema: ”Ee mwanadamu! Lau utanijilia na makosa yanayokaribia kujaa ulimwengu kisha ukakutana Nami pasi na kunishirikisha na chochote basi nitakutana na wewe na msamaha mfano wake.”[2]

Hili ni kwa sababu ya Tawhiyd. Sisi hatuwahimizi watu kufanya maasi. Tunawatahadharisha ukweli wa kuwatahadharisha, lakini tunabainisha umuhimu wa Tawhiyd. Sambamba na hilo tunabainisha ubovu wa linganizi za watu hawa wajinga walioghafilika. Hawajui ukhatari wa shirki. Hawaelewi dini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yeyote ambaye Allaah anamtakia kheri basi humpa ufahamu akaielewa dini.”[3]

Endapo wangelikuwa wanaifahamu dini ya Allaah, basi wangelielewa Kitabu cha Allaah, ulinganizi wa Mitume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na historia yake na namna walivyokuwa wanaipa umuhimu Tawhiyd, basi wasingekuja na upumbavu na utapeli huu ambao hautoki isipokuwa kwa watu wasiojua ulinganizi wa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja wanatukana ulinganizi wa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam).

Utapotazama namna ambavyo watu hawa wanalingania hutoona isipokuwa mapambo katika kulingania kwao. Pindi mjinga katika wao anasoma ulinganizi wa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) anaona kuwa si chochote si lolote ukilinganisha na mapambo ya watu hawa. Lakini mapambo yote haya ni matupu. Muda unavyokwenda yanapotea na kunabaki uhakika; uhakika wa ulinganizi wa Mitume. Inajaa ardhi na mbingu hata kama inahusu Tawhiyd peke yake:

”Lau mbingu saba na wakazi wake nikiondolewa Mimi na ardhi saba zikiwekwa kwenye sahani la mzani na ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” ikawekwa kwenye sahani la mzani, basi ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” ingelikuwa na uzito zaidi.”[4]

Fahamu uzito wa shahaadah, enyi masikini.

[1] 25:23

[2] at-Tirmidhiy (3540) ambaye amesema kuwa ni nzuri.

[3] al-Bukhaariy (71).

[4] Ahmad (2/169). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (134).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kashf-us-Sitaar, uk. 78-81
  • Imechapishwa: 28/11/2023