Swali: Ni ipi hukumu ya mapambo kwa aina ya sanamu kinyago?

Jibu: Vito hivi vinavyokuwa katika umbo la nyoka, kipepeo, mnyama, binadamu na mfano wake ni haramu. Haijuzu kuviuza wala kuvinunua. Ni haramu kwa makampuni kuuza vitu kama hivi wala kwa watengenezaji kuvitengeneza. Wale wenye kuvitengeneza wameingia ndani ya matishio yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kila mtengeneza picha atakuwa Motoni. Ataifanya kila picha aliyoitengeneza kuwa na nafsi ambapo ataadhibiwa kwayo Motoni.”[1]

Ni lazima kwa watengeneza masanamu vinyago hivi kumcha Allaah juu ya nafsi zao na juu ya ndugu zao waislamu. Ni wajibu kwa mamlaka na wahusika kuyazuia mambo hayo, kwa sababu ni haramu. Haijuzu kwa wanawake kuvivaa, si ndani ya swalah wala nje yake. Yule ambaye ana kitu katika vito hivyo anatakiwa kuvibadilisha, ima kwa kuondosha kichwa cha kinyago hicho au kukiparua kiasi cha kwamba kisitambulike.

[1] Muslim (2110).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/354-355)
  • Imechapishwa: 06/05/2026