Dr Ibraahiym [ar-Ruhayliy] amesema:

”Ni watu wangapi wa kawaida ambao wamefitinika na kuchanganyikiwa na kuingiwa na mashaka juu ya misingi ya dini kwa sababu ya kusoma vitabu vya Ruduud ambavyo akili zao hazivifahamu? Kwa ajili hiyo wamche Allaah wale ambao wanapambana kueneza vitabu hivi kati yao na watadhari wasiwe ni sababu ya kuwatia watu mtihani katika dini ya Allaah.”[1]

Unakusudia nini kwa ”vitabu vya Ruduud” ambavyo vimewafanya watu kuingiwa na mashaka na kusita? Unakusudia vitabu vya Ruduud dhidi ya watu wa batili, wazushi na watu wa fitina? Katika hali hiyo ni jambo linaloingia akili na ndio uhakika wa mambo. Sababu iliopelekea watu wengi kupotea ni kusambaa vitabu vya watu wa batili, ni mamoja wakati wanawaporaddi Ahl-us-Sunnah, kama mfano wa vitabu vya Dahlaan, an-Nabhaaniy, Raafidhwah, al-Ikhwaan al-Muslimuun, au vitabu vilivyoandikwa na watu waliojivisha vazi la Sunnah na kuwatetea watu wa batili na kuwapiga vita Ahl-us-Sunnah.

Na ikiwa unakusudia vitabu vya Ahl-us-Sunnah ambao wanawaraddi watu wa batili, basi ni maneno ya ajabu uliyosema na ni balaa. Ndani ya Qur-aan kuna Ruduud ngapi kwa wapotofu, mayahudi, manaswara na wanafiki?

Salaf waliandika vitabu vya Ruduud kuanzia wakati wa Imaam Ahmad, wanafunzi wake na wanafunzi wa wanafunzi wake. Hali iliendelea hivo mpaka wakati wa Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na wanafunzi wake kwenda mpaka wakati wa Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab na wanafunzi wake. Hali ikaendelea hivo mpaka hii leo. Ruduud hizo zimejaa ulimwenguni kote.

Ni wangapi ambao Allaah amewaongoza kupitia vitabu hivi? Ni Ahl-us-Sunnah wangapi ambao Allaah amewahifadhi kuingia ndani ya mashaka, upindaji na mitego ya Ahl-ul-Ahwaa´ kupitia vitabu hivi? Kuanzia hapa Salaf wamesema:

”Kuwaraddi Ahl-ul-Bid´ah ni jihaad.”

Baadhi wamesema:

”Kuwaraddi Ahl-ul-Bid´ah ni bora kuliko kupambana na silaha.”

Kupiga vita vitabu vya Ahl-us-Sunnah vilivyoandikwa hii leo ni jambo limeanzwa na al-Ikhwaan al-Muslimuun. Wanaeneza maoni batili, ´Aqiydah mbovu, vitabu vya upotofu na matusi ya kidhulumu kwa Ahl-us-Sunnah. Wakati baadhi ya Ahl-us-Sunnah walipoanza kuraddi batili, fitina na vitimbi vyao ndipo wakaweka ndani akili za watu kuwaponda wale wenye kuraddi na vitabu vya Ruduud.

Miongoni mwa mambo yenye kushangaza ni kuona kuna baadhi ya Ahl-us-Sunnah ambao wanakariri yale matusi ambayo yamepandikizwa na al-Ikhwaan al-Muslimuun katika kutukana vitabu vya Ruduud na kuwakaripia Ahl-ul-Bid´ah na watu wa fitina na wapotofu. Nataraji daktari atajirejea kutokana na maneno yake haya ya khatari bali kuwakemea wale wanaorudiarudia maneno mfano wa maneno yake.

[1] Uk. 33.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan maa fiy Naswiyhati Ibraahiym ar-Ruhayliy min al-Khalal wal-Ikhlaal, uk. 57-58
  • Imechapishwa: 10/12/2022