Vidhibiti vine kwa wanawake katika Ramadhaan

Swali: Ni vidhibiti vyepi ambavyo wanawake wa Kiislamu wanatakiwa kushikamana navyo katika mwezi huu?

Jibu: Vidhibiti vyepi ambavyo wanawake wa Kiislamu wanatakiwa kushikamana navyo katika mwezi huu mtukufu ni vifuatavyo:

1- Kutekeleza swawm kwa njia kamilifu zaidi kwa kuzingatia ya kwamba ni nguzo moja wapo ya Uislamu. Akifikwa na kikwazo chenye kumzuia kufunga kama hedhi, damu ya uzazi au vyengine vyenye kumtia uzito wa kufunga kama maradhi, safari, ujauzito au unyonyeshaji, basi ale na wakati huo huo aazimie kulipa siku zake katika siku nyenginezo.

2- Kulazimiana na kumdhukuru Allaah kukiwemo kusoma Qur-aan, kusema “Subhaan Allaah”, “Laa ilaaha illa Allaah”, “Alhamdulillaah”, “Allaahu Akbar”, kuswali swalah zote za faradhi kwa nyakati zake na aswali swalah za sunnah kwa wingi katika zile nyakati ambazo hazikukatazwa.

3- Kuuchunga ulimi kutokamana na maneno ya haramu kama vile usengenyi, uvumi, uongo, maapizo, matusi, kuyashusha macho kutokamana kutazama vitu vya haramu kama filamu za uchafu, picha chafu na kuwatazama wanaume kwa matamanio.

4- Kubaki majumbani na kutotoka isipokuwa kwa haja pamoja na kujisitiri, kuwa na heshima, kuwa na haya, kutochanganyikana na wanaume na kuzungumza nao kifitina ima moja kwa moja au kwa njia ya simu. Amesema (Ta´ala):

فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا

“Hivyo basi msilegeze maneno asije akaingiwa na tamaa ambaye moyoni mwake mna maradhi na semeni kauli inayokubalika.” (33:32)

Hakika baadhi ya wanawake au wengi wao wanaenda kinyume na adabu za Kishari´ah katika Ramadhaan na nje yake ambapo wanatoka kwenda masokoni hali kujipamba kikamilifu na kujitia manukato na hawajisitiri vile itakikavyo. Wanafanya mzaha na wamiliki wa maduka, wanawaonyesha nyuso zao, au wanaweka kizuizi kisichositiri na wanaonyesha vilevile mikono yao. Haya ni haramu na ni yenye kuvutia katika fitina. Dhambi zake katika Ramadhaan ni khatari zaidi kutokana na utukufu wa mwezi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaam al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alfawzan.af.org.sa/node/14891
  • Imechapishwa: 17/06/2017