Uwajibu wa kuitakasa nia katika ´ibaadah zote

Ni wajibu kwa mtu amtakasie nia yake Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa ´ibaadah zake zote. Asinuie kwa ´ibaadah zake isipokuwa Uso wa Allaah na Nyumba ya Peponi. Hili ndilo ambalo Allaah ametuamrisha. Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini.”

bi maana kwa kumtakasia matendo.

وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“… wasimamishe swalah na watoe zakaah, na hiyo ndiyo dini iliyosimama sawasawa.” (98:05)

Inatakikana vilevile aihudhurishe nia, bi maana nia ya Ikhlaasw, katika ´ibaadah zote. Kwa mfano tukija katika wudhuu´ anuie kuwa ametawadha kwa ajili ya Allaah na ametawadha kwa kutekeleza amri ya Allaah. Haya ni mambo matatu:

1- Ni ya ´ibaadah.

2- Nia iwe kwa ajili ya Allaah.

3- Nia juu ya kwamba amefanya hivo kwa kutekeleza amri ya Allaah.

Hii ndio nia kamilifu zaidi.

Vivyo hivyo iwe katika swalah:

1- Nuia kama unaswali dhuhr, ´aswr, maghrib, ´ishaa au fajr na mfano wa hayo.

2- Nuia vilevile ya kwamba unaswali kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall). Isiwe unaswali kwa ajili ya jambo jengine. Sio unaswali kwa ajili ya kujionyesha wala kutaka kusikika. Sio unaswali ili usifiwe kwa ajili ya swalah yako au ili uweze kupata kitu katika mali au maslahi ya kidunia.

3- Zivute hisia ya kwamba unaswali kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mola Wako. Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ

“Wakasimamisha swalah.” (02:277)

فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ

“Mtakapopata utulivu, basi simamisheni swalah. Kwani swalah kwa waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu.” (04:103)

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ

“Simamisheni swalah na toeni zakaah” (02:110)

Vilevile maamrisho mengineyo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/13-14)
  • Imechapishwa: 26/12/2017