Miongoni mwa adabu ambazo zinatakiwa kuchungwa wakati wa kuuliza ni muulizaji asiwaulize wanazuoni juu ya kitu ambacho tayari anajua majibu yake. Baadhi ya wanafunzi au watu ambao wana maarifa kiasi anakuwa tayari amekwishafanya utafiti na ameshajua maoni mbalimbali ya mada fulani, baadaye anakuja kuuliza. Baada ya kuuliza na jibu likaafikiana na moja ya maoni aliyoyasoma, anaanza kuleta vipingamizi kama kumuuliza dalili ya hicho alichosema na kwamba dalili hiyo imekosolewa kwa njia hii, kwamba wanazuoni wengine wamesema hivi na mfano wa hayo. Kuna tofauti kati ya kuuliza kwa lengo la kufaidika na kujua ikiwa ulikuwa hujui, na kati ya kufanya majadiliano na mwanachuoni au mwalimu ambaye si kazi yake wala hajakufungulia mlango wa kujadiliana naye. Mwambie kabla kwamba unataka kujadiliana naye juu ya masuala fulani ili kijulikane kile kilichoko kwangu na kilijulikane kile kilichoko kwako na hatimaye tuweze kuifikia haki. Vinginevyo ni kitu kisichotakikana kwa sababu ni kutokuwa na adabu na wanazuoni. Ni kukiuka haki ya mwanachuoni. Isipokuwa ikiwa umetangulia kumwambia kuwa unataka kutafiti naye masuala haya, akikupa idhini ya kufanya hivo ndipo unaweza kufanya hivo.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ‘Abdil-‘Aziyz Aalish-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muhadhara: Adab-us-Suwaal https://saleh.af.org.sa/sites/default/files/2017-11/006.mp3
  • Imechapishwa: 12/01/2023