Upasuaji wa matiti, midomo na uso

Swali: Baadhi ya madaktari wa upasuaji wa plastiki huwafanyia wanawake upasuaji ambapo wanainua uso, kuupanua au kupunguza midomo, pamoja na kuyafanya makubwa, kuyapanua au kuyapunguza matiti. Je, inafaa kwa wanawake  kuwaendea madaktari hawa kama hakuna dharurah? Je, operesheni hizi ina maana ya kubadilisha maumbile ya Allaah? Je, inafaa kwa madaktari hawa wa plastiki kupasua namna hii? Je, inafaa kuwafanyia matangazo madaktari hawa?

Jibu: Operesheni zilizotajwa ni haramu kwa sababu ni kubadilisha maumbile ya Allaah (Ta´ala). Mambo hayo yamefanana na kuchonga nyusi, kujichanja na kutia mwanya. ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amemlaani mwanamke mwenye kufanya chanjo na mwanamke mwenye kufanywa chanjo, mwanamke mwenye kuchonga nyusi na mwanamke mwenye kuchongwa nyusi na mwanamke mwenye kufanya mwanya kwa ajili ya kutafuta urembo wanaoyabadilisha maumbile ya Allaah.”

Kisha akasema:

“Je, nisimlaani yule aliyelaaniwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndani ya Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall)?”[1]

Kwa hivyo daktari anatakiwa kutadhari kufanya upasuaji aina hizi, amche Allaah, Mola wake, na afanye upasuaji ambao ni halali. Kichache ambacho ni halali ni bora kuliko kingi ambacho ni haramu.

Na wala haijuzu kufanya matangazo ya operesheni kama hizi kwa sababu kitebdo hicho ni kushirikina katika dhambi na uadui, jambo ambalo limekatazwa na Allaah (Ta´ala). Ni haramu kwa wanawake kufanya operesheni kama hizo. Ni juu yao kumcha Allaah  juu ya nafsi zao na juu ya wanawake wengine wote. Si halali kwa wasimamizi wa wanawake kuanzia baba zao, waume zao na wengineo kuwaacha wakafanya operesheni kama hizi. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ

”Jikingeni nafsi zenu na familia zenu na Moto ambao mafutayake ni watu na mawe.”[2]

Namwomba Allaah azitengeneze hali za waislamu na awakinge kutokamana na sababu ya hasira na adhabu Yake. Kwani hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa, Mkarimu.

1420-07-28

[1] al-Bukhaariy (5934) na Muslim (2125).

[2] 66:6

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/56-57)
  • Imechapishwa: 15/06/2026