Nijitolee figo na kupewa gari?

Swali: Je, inafaa kwa mtu kujitolea kumpa mgonjwa figo yake moja na akawaomba familia ya mgonjwa huyo wampe yule mtoaji baadhi ya mali kama vile gari kwa vile hali yake itabadilika baada ya kupewa figo hiyo?

Jibu: Kamati ya Kibaar-ul-´Ulamaa wametoa fatwa juu ya kwamba inafaa kufanya hivo. Hata hivyo sioni kufaa kufanya hivo. Viungo vya mwanadamu ni amana. Hanaabilah (Rahimahu Allaah) wanaona kutokufaa kujitolea viungo ingawa mtu aliacha anausia kufanywe hivo baada ya kufa kwake. Hata kama kuna uwezekano kupeana viungo huko kukafulu kwa asimilia 90, lakini madhara ya kupeana viungo ni yenye uhakika, kukiwemo kupeana mafigo. Ni kweli kwamba mwili unaweza kufanya kazi kwa figo moja, lakini kufanya kwake kazi sio kama ulipokuwa na mafigo mawili. Kwa sababu Allaah hajaumba chochote burebure tu. Jengine ni kwamba endapo figo moja hii itafeli, mtu anakufa. Endapo angelikuwa na mafigo mawili asingekufa. Kwa ajili hiyo mimi naona kutofaa kitendo hicho tofauti na jambo la kupeana damu. Jambo la kupeana damu kunaingia mahali pake damu nyingine. isitoshe yule mwenye kupeana damu hadhuriki na wala hapotezi kiungo cha mwili.

Licha ya hvio sioni kama kuna tatizo kwa yule mwenye kuchukua maoni ya kamati. Suala hili limejengeka juu ya ijtihaad na kwa ajili hiyo mtu hawezi kumlazimisha mwengine maoni yake. Lakini kwa vile haifai kwangu kuficha elimu niliyopewa na Allaah ndio maana nikalibaisha hapa. Vinginevyo ningaweza kusema kuwa baraza limeshatoa fatwa na hivyo nikawarejesha watu huko. Lakini kwa kuzingatia kwamba elimu ni amana na mtu hajui atakutana na Allaah (´Azza wa Jall) akiwa na hali gani, ndipo nikaona kuwa ni lazima kubainisha kile ninachokijua. Namwomba Allaah (Ta´ala) kwa idhini Yake atuongoze sote katika ile haki ambayo watu wametofautiana juu yake. Kitabu cha Hanaabilah “al-Iqnaa´” kilichotangaa kumetajwa yafuatayo:

“Haijuzu kwa hali yoyote kuhamisha kiungo cha mwili cha mtu hata kama mwenye kujitolea atausia kufanywe hivo baada ya kufa kwake.”

Kwa maana ya kwamba endapo yule mwenye kujitolea atasema nikifa basi fulani apewe figo, mkono wangu au kiungo kingine.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/51-53)
  • Imechapishwa: 15/06/2026