40 – Abu ´Amr Ahmad bin Muhammad bin Ibraahiym, mtumwa wa Banuu Haashim aliyeachwa huru, ametukhabarisha: Abu Umayyah at-Tarsuusiy ametuhadithia: Abul-Waliyd ametuhadithia: ´Ikrimah bin ´Ammaar ametuhadithia: Yahyaa bin Abiy Kathiyr ametuhadithia, kutoka kwa Abu Salamah: Abu Hurayrah amenihadithia kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Aadam na Muusa walizozana ambapo Aadam akamwambia Muusa: ”Wewe ndiye ambaye Allaah amekuteua juu ya viumbe Wake na akakufadhilisha kwa ujumbe Wake. Kisha ukafanya uliyoyafanya na ukaua mtu.” Muusa akamwambia Aadam: ”Wewe ndiye Aadam ambaye Allaah amekuumba kwa mkono Wake, akawafanya Malaika Wake kukusujudia na akakukaza Pepo Yake. Kisha ukafanya yale uliyoyafanya. Usingeyafanya basi kizazi chako kingeliingia Peponi.” Ndipo Aadam akasema: ”Je, unanilaumu kwa jambo ambalo nilikadiriwa kabla ya kuumbwa?” Aadam akamshinda Muusa.”

41 – Muhammad bin al-Husayn al-Qattwaan ametukhabarisha huko Neyshabur: Ahmad bin Yuusuf as-Sulamiy ametuhadithia: Muhammad bin an-Nadhwr al-Jarashiy ametuhadithia: ´Ikrimah bin ´Ammaar ametuhadithia: Yahyaa bin Abiy Kathiyr ametuhadithia: Abu Salamah ametuhadithia… ´Ikrimah bin ´Ammaar pia amesema: Nimeyasikia hayo kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Umayr al-Laythiy, kutoka kwa Abu Hurayrah, ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Aadam na Muusa walizozana. Aadam akasema: ”Ee Muusa, wewe ndiye amekutumiliza kwa ujumbe Wake na akakuteua kwa maneno Yake juu ya viumbe Wake. Kisha ukafanya kadhaa na kadhaa.” Muusa akasema: ”Ee Aadam, wewe ndiye Aadam, baba wa watu ambaye Allaah (Jalla wa ´Azz) amekuumba kwa mkono Wake, akawafanya Malaika Wake kukusujudia na akakukaza Pepo Yake. Kisha ukafanya yale uliyoyafanya. Usingeyafanya basi kizazi chako kingeliingia Peponi.” Ndipo Aadam akamwambia Muusa: ”Je, unanilaumu kwa jambo ambalo nilikadiriwa kabla ya kuumbwa?” Aadam akamshinda Muusa.”

42 – Abu ´Amr ametukhabarisha: Abu Umayyah ametuhadithia: Haamid bin Yahyaa ametuhadithia, kutoka kwa Ayyuub bin an-Najjaar al-Yamaamiy: Yahyaa bin Abiy Kathiyr ametuhadithia, kutoka kwa Abu Salamah, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

”Aadam na Muusa walizozana. Muusa akasema: ”Ee Aadam, wewe ndiye baba yetu ambaye Allaah amekuumba kwa mkono Wake, akakukaza Pepo Yake na akawafanya Malaika Wake kukusujudia, ambapo ukasababisha tukaangamia na kutolewa Peponi.” Aadam akasema: ”Wewe ndiye Muusa ambaye Allaah amekuzungumzisha maneno kikweli, akakuandikia Tawraat kwa mkono Wake na akakuteua kwa ujumbe Wake. Ni lini uliona ndani ya Kitabu cha Allaah (Ta´ala) imeandikwa:

وَعَصَىٰ آدَمُ رَبَّهُ فَغَوَىٰ

”Aadam akamuasi Mola Wake akapotoka.”[1]?

Akasema: ”Miaka arobaini kabla.” Akasema: ” ”Je, unanilaumu kwa kufanya jambo ambalo Allaah alinikadiria miaka arobaini kulifanya kabla ya Yeye kuniumba?” Aadam akamshinda Muusa.”

Hadiyth hizi ni Swahiyh na zimethibiti na haziwezi kutupiliwa mbali. Hadiyth hizi zimepokelewa kupitia njia  nyingi kutoka kwa Abu Hurayrah, ikiwa ni pamoja vilevile na Abu Salamah, Muhammad bin Siyriyn, al-A´raj na Sa´iyd bin al-Musayyab.

[1] 20:121

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ishaaq bin Mandah (afk. 395)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah, uk. 69-72
  • Imechapishwa: 15/06/2026
  • Taaliki: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy