Uongo wa as-Saqqaaf juu ya Ibn Khuzaymah

Sababu nyingine inayowafanya watu kunitukana ni kutaka na kupenda kuonekana na umaarufu. Sababu hizi zinapatikana kwa watu wengi. Mmoja wao ni yule anayeitwa Hasan as-Saqqaaf. Hakuna yeyote ambaye alikuwa akilisikia jina lake hapo kabla. Radd yake ikafanya jina lake kuwa maarufu, hata kama itapelekea kuitukana Sunnah na Ahl-us-Sunnah. Miongoni mwa maajabu ni kuwa anajidai kuwa ni Suufiy ilihali Suufiyyah iko kinyume naye. Kwani hakika miongoni mwa madhehebu yao ni kujiweka chini na sio kutafuta umaarufu. Mmoja wa wakale wao amesema:

“Kuwa mkia na usiwe kichwa.”

Ukiongezea juu ya hilo ni kwamba ana ´Aqiydah ya mapote ya wale waliokuja nyuma. Ni Mu´taziliy ambaye anapinga sifa za kiungu na anawachafua maimamu wa waumini na wafuasi wao – na mimi ni mmoja katika wao na himdi zote ni stahiki ya Allaah – katika taaliki zake ambazo amekichafua kitabu cha Ibn-ul-Jawziy  ”Daf´ Shubah-it-Tashbiyh”. Aidha anawazulia uongo mbalimbali. Endapo ningetaja uongo wake wote, basi ungelienea katika mjeledi. Hebu tupige mfano mmoja anasema katika taaliki zake:

“Haafidhw Ibn Khuzaymah amejutia kuandika kitabu chake “at-Tawhiyd”, kama ambavo unaweza kuliona hilo katika kitabu cha “al-Asmaa´ was-Swiffaat”, uk. 267, cha al-Bayhaqiy.

Huu ni uongo uliochanganywachanganywa. Katu Ibn Khuzaymah hakujutia na wala al-Bayhaqiy hakuyanasibisha hayo kwake. Ni vipi inaingia akilini kwamba Ibn Khuzaymah amejutia juu ya kitabu chake “at-Tawhiyd” ilihali ni kitabu cha Tawhiyd safi? Ni vipi inaingia akilini kwamba al-Bayhaqiy anaweza kunakili kitu kama hicho? Huu ni uongo mkubwa kabisa.

Ukirejea katika ukurasa uliotajwa katika “al-Asmaa´ was-Swiffaat”, hutoona uzushi uliyozuliwa. Kilichoko ni yeye Ibn Khuzaymah anakiri kwamba hakuwa mwenye kujua elimu ya falsafa. Hayo ni katika kisa kilichopokea al-Bayhaqiy ikiwa kimesihi. Simjui ni nani huyu Abul-Fadhwl al-Batwaayiyniy. as-Sam´aaniy hakumtaja katika “al-Answaab”. Allaah ndiye mjuzi zaidi wa kumjua.

Ikiwa kweli imesihi kwamba Ibn Khuzaymah alikiri hilo, si jambo lenye kumtia kasoro, kama anavofikiria mjinga huyu mwenye malengo mabaya. Bali ni jambo linalomnyanyua daraja na kuongeza ubora wake. Kwani hakika katika kufanya hivo anacho kiigizo chema kwa Salaf na maimamu wanne na wale wenye kuwafuata kwa wema. Kwa yakini kabisa hakukuwa kati yao wasomi wa falasafa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naasir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (1/4-5)
  • Imechapishwa: 18/08/2020