Kuamrisha mema na kukataza maovu katika hajj

Swali: Baadhi ya watu pindi wanapotekeleza ´ibaadah za hajj wanachukulia wepesi jambo la kuamrisha mema na kukataza maovu ambapo wanaona maovu na wala hawayakatazi na mema hawayaamrishi. Unapowauliza juu ya hilo wanasema kwamba Allaah anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ ۖ لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ

“Enyi mlioamini! Ni juu yenu [majukumu ya] nafsi zenu. Hawakudhuruni waliopotoka, ikiwa mmeongoka.” (05:105)

Unasemaje juu ya hili? Ni ipi tafsiri ya Aayah hiyo?

Jibu: Maoni yangu juu ya hili ni kwamba ni lazima kwa kila mtu kuamrisha mema na kukataza maovu. Ni mamoja katika hajj au kwenginepo. Kwa sababu maandiko ni yenye kuenea. Lakini katika hajj huenda jambo likawa na mkazo zaidi. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِي الْحَجِّ

”Asifanye tendo la ndoa wala ufasiki wala ubishi katika Hajj.” (02:197)

Kuhusu Aayah tukufu ambapo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ ۖ لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ

“Enyi mlioamini! Ni juu yenu [majukumu ya] nafsi zenu. Hawakudhuruni waliopotoka, ikiwa mmeongoka.”

Yule asiyeamrisha mema na kukataza maovu anapostahiki hakuongoka. Lakini mtu asipoweza kuamrisha mema na kukataza maovu asijichoshe. Bali aichunge nafsi yake. Hatomdhuru yule mwenye kupotea. Tafsiri ya Aayah ni hii. Kwa ajili hii Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Enyi watu! Hakika nyinyi mnasoma Aayah hii:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ ۖ لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ

“Enyi mlioamini! Ni juu yenu [majukumu ya] nafsi zenu. Hawakudhuruni waliopotoka, ikiwa mmeongoka.”

Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu watakapoona maovu na wasiyazuie, basi Allaah anakaribia kuwateremshia adhabu – au alisema – kuwateremshia adhabu kutoka Kwake.”

Aayah iko wazi:

لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ

“Hawakudhuruni waliopotoka… “

Kwa sharti:

إِذَا اهْتَدَيْتُمْ

“… ikiwa mmeongoka.”

Mwenye kuacha kuamrisha mema na kukataza maovu panapostahiki basi hakuongoka.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (73) http://binothaimeen.net/content/1694
  • Imechapishwa: 18/08/2020