Ulinganizi wa Ahl-us-Sunnah jana ndio ulinganizi wa Ahl-us-Sunnah leo, kwa maana nyingine ni ulingani uliojengeka juu ya Qur-aan na Sunnah kwenda katika Qur-aan na Sunnah. Ni ulingano katika elimu yenye manufaa kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote ambaye Allaah anamtakia kheri, basi humpa ufahamu katika dini.”[1]

Elimu yenye manufaa ndio ambayo ilikuwa ni sababu ya kuwanufaisha waislamu wengi kwa ulinganizi huu uliobarikiwa. Abu Muusa (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfano wa kile ambacho amenitumiliza kwacho Allaah katika uongofu na elimu ni kama mfano wa mvua iliyotua juu ya ardhi. Ikapatikana katika ardhi hiyo kipande kizuri; kikayakubali na kuyapokea yale maji na kuotesha majani na nyasi nyingi. Kukapatikana kipande kingine kikavu; kiliyazuia maji na Allaah akawanufaisha watu kwayo. Wakanywa kutoka katika maji hayo, wakanywesheleza na wakalima. Kipande kingine ikawa ni changaforo; ikawa haizuii maji na wala haitoshi majani. Huyo ni mfano wa yule aliyeifahamu dini ya Allaah (Ta´ala) na  Allaah akamnufaisha kwa yale niliyotumilizwa nayo; amejifunza na yeye akafunza. Na mfano wa yule ambaye hakunyanyua kwa hiyo elimu kichwa chake na wala hakukubali uongofu wa Allaah ambao mimi nimetumilizwa nao.”[2]

Ulinganizi wa Ahl-us-Sunnah sio ulinganizi wa vurugu. Ulinganizi wa Ahl-us-Sunnah sio wa kivyamavyama. Ulinganizi wa Ahl-us-Sunnah ni kama tulivosema ni wenye kuiponya mioyo yetu yenye maradhi. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ

“Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rehema kwa waumini.”[3]

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ

“Enyi watu! Hakika yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu na ponyo ya yale yote yaliyomo vifuani na mwongozo na rehema kwa waumini.”[4]

Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye amewanufaisha waislamu wengi kwa ulingano huu. Hiyo ni fadhilah za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Sisi ni wahitaji wa ulinganizi huu zaidi kuliko ambavo unavotuhitaji sisi. Yule anayelingania kwa Allaah basi Allaah (´Azza wa Jall) humnyanyua:

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ

“Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania watu kwa Allaah na akatenda mema na akasema: “Hakika mimi ni miongoni mwa waislamu?”[5]

Ni ngazi tukufu na ni jukumu la Mitume:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ شَاهِدًا وَمُبَشِّرًا وَنَذِيرًا وَدَاعِيًا إِلَى اللَّـهِ بِإِذْنِهِ وَسِرَاجًا مُّنِيرًا

“Ee Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiriaji na mwonyaji na mlinganiaji kwa Allaah kwa idhini Yake na taa lenye kuangaza.”[6]

[1] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (67).

[2] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (76).

[3] 17:82

[4] 10:57

[5] 41:33

[6] 33:45-46

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Mu´aanid, uk. 39-40
  • Imechapishwa: 30/01/2025