“Ukipenda baki na wanangu au nikutaliki?”        

Swali: Unasemaje kwa yale yanayosemwa na baadhi ya waume pindi wanapooa mke mwengine wanamwambia yule mke wa kwanza:

“Uko na khiyari ima ya kuomba talaka au kubaki na wanangu.”

Je, kuna neno endapo mke hatomjibu kitu? Ni vipi hali ya mwanamke huyu ambaye hakumjibu?

Jibu: Kwanza inatusikitisha sana kuona kuna baadhi ya wanawake pindi waume zao wanapooa mke mwengine, basi wanafanya mambo yasiyomstahikia kama kupiga makelele, ususaji, chuki, kumuomba mume ima amtaliki yeye au yule mke mpya na mfano wa hayo.

Kinachotakiwa kwa mwanamke ni yeye ajisahilishie jambo hili. Kitu hichi kilitokea kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), viongozi wa waumini katika Maswahabah, Taabi´uun na mpaka hii leo. Ikiwa Allaah kamjuzishia mwanaume kuoa mwanamke mmoja hadi wanne, Yeye ndiye mjuzi zaidi, mwenye hekima zaidi na mwenye huruma zaidi. Hivyo inatakiwa kwa mwanamke ajiwepesishie suala hili. Anatakiwa awe na subira juu ya ule uzito anaopata na asimuombe mume wake kitu. Bila ya shaka mwanaume atakuwa mlaini endapo yule mke wake wa kwanza naye atakuwa mlaini. Lakini baadhi ya wanawake pindi waume zao wanaoa juu yao, basi wanawalazimisha na kuwaomba mambo wanayoyachukia. Hapo ndipo mume humwambia mwanamke:

“Ukipenda utabaki na watoto wako pamoja na mimi na kama wataka nakutaliki.”

Akisema hivi haina neno. Kwa sababu huu ndio uhakika wa mambo.

Pindi Sawdaa bint Zam´ah alipokuwa mtumzima ambaye ni mmoja katika mama wa waumini na akaona kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hamjali sana, alikuwa mwerevu. Alichofanya ni kumpa siku yake ´Aaishah mama wa waumini. Alielewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anampenda ´Aaishah. Hivyo akajitolea siku yake kumpa ´Aiashah na yeye akabaki hana zamu. Lakini hata hivyo akabaki kuwa ni mama wa waumini (Radhiya Allaahu ´anhaa).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (02)
  • Imechapishwa: 02/05/2020