Miongoni mwa sifa anazosifika nazo ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ni kwamba alikuwa mkali dhidi ya wanafiki, washirikina na waislamu wanaoenda kinyume. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ee ´Umar! Naapa kwa ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake hujashika njia yoyote isipokuwa shaytwaan hushika njia nyingine mbali na ile uliyoshika.”[1]

Ukali dhidi ya Ahl-ul-Bid´ah na watu wa batili ilikuwa ni fadhilah kwa maimamu wengi. Yule ambaye alikuwa anafanya ukali kwa Ahl-ul-Bid´ah hawakuwa wakimpiga vita. Hawakuwa wakimdharau. Hawapingani naye. Bali walikuwa wakifanya ni miongoni mwa ubora wake na sifa zake za kipekee. ´Abdullaah bin al-Mubaarak amesema:

”Sijamuona mtu baada ya kile kizazi cha kwanza kama Hammaad bin Salamah.”

Wuhayb bin Khaalid amesema:

”Hammaad bin Salamah alikuwa ndiye bwana na mjuzi wetu zaidi.”

Wengine wamesema:

”Alikuwa ni imaam katika kisomo cha Qur-aan, Hadiyth na kiarabu. Alikuwa ni Faqiyh mfaswaha. Alikuwa ni imaam katika Sunnah na miongoni mwa wale wa mwanzo walioandika vitabu.”

Amesifiwa sana. al-´Ijliy amesema:

“Alikuwa akiaminika na alikuwa anazingatiwa ni mmoja katika Ahl-ul-Hadiyth wenye hekima.”

Imaam ´Aliy al-Madiyniy amesema:

“Mimi namuona kuwa ni hoja inapokuja katika elimu ya wanamme. Yeye ndiye mjuzi zaidi juu ya Thaabit al-Bunaaniy na ´Ammaar bin Abiy ´Ammaar. Mwenye kumzungumza vibaya Hammaad bin Salamah basi itilie shaka dini yake.”

Ibn Hibbaan amesema:

”Hakuna yeyote katika wale marafiki zake Hammaad Baswrah aliyekuwa mfano wake inapokuja katika ubora, dini, ´ibaadah, elimu, uandishi, kukusanya na uimara katika Sunnah na kuwaraddi Ahl-ul-Bid´ah. Hakuna yeyote katika wakati wake ambaye alikuwa akimzungumza vibaya isipokuwa Mu´taziliy na Qadariy au Jahmiy mzushi. Sababu ni kwa kuwa alikuwa akidhihirisha ile Sunnah Swahiyh inayopingwa na Mu´tazilah.”

Imaam Ahmad bin Hanbal amesema:

”Ukimuona mtu anamzungumza vibaya Hammaad bin Salamah basi utilie shaka Uislamu wake. Kwa sababu alikuwa mkali kwa wazushi.”

Sifa ni nyingi juu ya Hammad bin Salamah. Ambaye atarejea vitabu vya maimamu ambapo ndani yake wamebainisha ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah na I´tiqaad mbovu za Ahl-ul-Bid´ah basi ataona jinsi mara nyingi wanazungumza maneno makali kuhusu Ahl-ul-Bid´ah, makundi na mtu mmojammoja. Humo hatoona mtindo wa masharti na vigezo vya Dr Ibraahiym [ar-Ruhayliy] ambavyo vinafanya takriban ni jambo lisilowezekana kuwaraddi Ahl-ul-Bid´ah na wale wenye kwenda kinyume. Hili khaswa kwa kuzingatia kuwa maumbile ya watu ni yenye kutofautiana. Ni nani anaweza kuwatia watu wote katika mkumbo mmoja? Mimi nadhani kuwa wa kwanza ambaye hawezi kutendea kazi sharti hizi na mfumo huu ni mwandishi wa nasaha hii.

Vyovyote vile ulaini na upole ni mambo yanayotakikana. Lakini visiponufaisha basi inatakiwa kutumia ukali kwa wale wanaofanya ukaidi na wanaopingana na haki na watu wa haki. Jambo kama hilo limefanyika mara nyingi ndani ya Qur-aan, Sunnah na matendo ya Salaf. Mtu kujifanya hajui jambo hilo ni khatari juu ya Uislamu na juu ya Ahl-us-Sunnah.

[1] al-Bukhaariy (3294) na Muslim (2396).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan maa fiy Naswiyhati Ibraahiym ar-Ruhayliy min al-Khalal wal-Ikhlaal, uk. 46-47
  • Imechapishwa: 10/12/2022