Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

45 – Qur-aan ni maneno ya Allaah.

MAELEZO

Baada ya kumuamini Allaah (´Azza wa Jall) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) unatakiwa kuamini kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah. Kwa sababu ndio Qur-aan ambayo amekuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah amemteremshia Qur-aan. Qur-aan hii sio katika maneno ya Muhammad wala maneno ya Jibriyl (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam); si venginevyo ni maneno ya Allaah. Allaah amezungumza kwayo, Jibriyl akaipokea kutoka kwa Allaah, Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameipokea kutoka kwa Jibriyl na Ummah wameipokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Qur-aan ni maneno ya Allaah, imetoka Kwake (Subhaanah). Jibriyl hakuichukua kutoka katika Ubao uliohifadhiwa, kama wanavosema wapotofu. Qur-aan ni maneno ya Mola wa walimwengu. Jibriyl na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) ni wafikishaji kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Maneno yanaegemezwa kwa yule aliyeyasema mwanzo, na si kwa yule aliyeyasema hali ya kuyafikisha. Yule mwenye kusema kuwa Jibriyl ameichukua Qur-aan kutoka katika Ubao uliohifadhiwa, au akasema kuwa Allaah aliiumba kwenye kitu ambapo Jibriyl akaichukua kutoka katika kitu hicho, ni kafiri. Hiyo ndio ´Aqiydah ya Jahmiyyah, Mu´tazilah na wanaowafata kichwa mchunga.

Qur-aan ni maneno ya Allaah ni mamoja herufi na maana yake. Allaah ameizungumza anavyotaka. Tunamsifu kuwa Allaah anazungumza. Maneno ni miongoni mwa sifa Zake za kimatendo. Hata hivyo hatujui ameyazungumza namna gani. Maana yake ni yenye kutambulika na namna gani sisi hatuitambui.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 66-67
  • Imechapishwa: 10/12/2022