Kwa hivyo ni lazima kuhusiana naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuamini mambo yafuatayo:

1 – Yeye ni mja na Mtume wa Allaah.

2 – Yeye ni Nabii wa mwisho na hakuna Nabii mwingine baada yake.

3 – Ujumbe wake ni wenye kuenea na ni kwa majini na watu. Dalili ya kwamba ametumilizwa kwa watu wote zimekwishatangulia. Dalili kwamba ametumwa kwa majini ni maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَإِذْ صَرَفْنَا إِلَيْكَ نَفَرًا مِّنَ الْجِنِّ يَسْتَمِعُونَ الْقُرْآنَ فَلَمَّا حَضَرُوهُ قَالُوا أَنصِتُوا ۖ فَلَمَّا قُضِيَ وَلَّوْا إِلَىٰ قَوْمِهِم مُّنذِرِينَ قَالُوا يَا قَوْمَنَا إِنَّا سَمِعْنَا كِتَابًا أُنزِلَ مِن بَعْدِ مُوسَىٰ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ وَإِلَىٰ طَرِيقٍ مُّسْتَقِيمٍ يَا قَوْمَنَا أَجِيبُوا دَاعِيَ اللَّـهِ وَآمِنُوا بِهِ يَغْفِرْ لَكُم مِّن ذُنُوبِكُمْ وَيُجِرْكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ 

”Wakati Tulipowaelekeza kwako kundi miongoni mwa majini wakisikiliza Qur-aan, walipoihudhuria walisema: “Nyamazeni [msikilize]!” Ilipokwisha [kusomwa], waligeuka kurudi kwa watu wao wakiwaonya. Wakasema: “Enyi qaumu yetu! Hakika sisi tumesikia [kunasomwa] Kitabu kilichoteremsha baada ya Muusa hali ya kuwa kinayasadikisha yaliyo kabla yake, kinaongoza katika haki na katika njia iliyonyooka. Enyi watu wetu! Mwitikieni mlinganiaji wa Allaah na mwaminini hivyo Atakusameheni madhambi yenu na atakukingeni na adhabu iumizayo.”[1]

Bi maana Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vilevile Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ أُوحِيَ إِلَيَّ أَنَّهُ اسْتَمَعَ نَفَرٌ مِّنَ الْجِنِّ فَقَالُوا إِنَّا سَمِعْنَا قُرْآنًا عَجَبًا يَهْدِي إِلَى الرُّشْدِ فَآمَنَّا بِهِ ۖ وَلَن نُّشْرِكَ بِرَبِّنَا أَحَدًا

“Sema: “Nimefunuliwa Wahy ya kwamba kundi miongoni mwa majini lilisikiliza, wakasema: “Hakika sisi tumeisikia Qur-aan ya kushangaza – inaongoza katik uongofu, hivyo basi tukaiamini na wala hatutomshirikisha Mola wetu na yeyote.”[2]

Ni dalili kuwa ujumbe wake ni kwa majini yote. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumwa kwa walimwengu wote; watu na majini. Yule mwenye kumuamini ataingia Peponi na ambaye hakumuamini ataingia Motoni, ni mamoja ni katika watu au majini.

Mtunzi wa kitabu amesema:

“… nuru na mwangaza… “

Ni visawe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumwa kwa yote mawili. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ شَاهِدًا وَمُبَشِّرًا وَنَذِيرًا وَدَاعِيًا إِلَى اللَّـهِ بِإِذْنِهِ وَسِرَاجًا مُّنِيرًا

“Ee Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiriaji na mwonyaji na mlinganiaji kwa Allaah kwa idhini Yake na taa lenye kuangaza.”[3]

[1] 46:29-31

[2] 72:1-2

[3] 33:45-46

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 65-66
  • Imechapishwa: 10/12/2022