Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

44 – Ametumilizwa kwa majini na watu wote kwa haki na uongofu, nuru na mwangaza.

MAELEZO

Haya pia ni lazima kuyaamini juu ya Mtume (Swalla Allaah ´alayhi wa sallam). Haitoshi peke yake kuamini kuwa yeye ni Mtume wa Allaah, bali yeye ni Mtume wa Allaah kwa majini na watu wote. Amesema (Subhaanah):

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَــكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

“Na Hatukukutuma isipokuwa kwa watu wote hali ya kuwa ni mbashiriaji na muonyaji, lakini watu wengi hawajui.”[1]

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

“Sema: “Hakika mimi ni Rasuli wa Allaah kwenu nyinyi nyote.”[2]

Kwa hivyo ujumbe wake ni kwa watu wote, kitu ambacho ni sifa yake ya kipekee (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ni Mtume wa watu wote na viumbe wote wamewajibishiwa kumtii; waarabu na wasiokuwa waarabu, weusi na weupe, majini na watu. Kila ambaye amefikiwa na ulinganizi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi analazimika kumtii na kumfuata. Baadhi ya manaswara wanasema kuwa ni Mtume wa waarabu peke yao. Msemo huu ni kumkufuru na kumkadhibisha Allaah (´Azza wa Jall) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwani Allaah anasema:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَــكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

“Na Hatukukutuma isipokuwa kwa watu wote hali ya kuwa ni mbashiriaji na muonyaji, lakini watu wengi hawajui.”[3]

تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَى عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا

“Amebarikika Yule ambaye ameteremsha Pambanuzi kwa mja Wake ili awe ni muonyaji kwa walimwengu.”[4]

Kwa hiyo ujumbe wake ni kwa walimwengu wote. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nabii alikuwa akitumwa kwa watu pekee ilihali mimi nimetumwa kwa watu wote.”[5]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatumia barua wafalme wa ulimwenguni akiwalingania katika Uislamu. Kwa hiyo ikafahamisha kuwa ametumilizwa kwa walimwengu wote ardhini. Ameamrisha kupambana jihaad ili watu waingie katika Uislamu. Kwa hiyo ikafahamisha kuwa ujumbe wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wenye kuenea. Kwa hivyo ni lazima kuamini jambo hilo.

[1] 34:28

[2] 7:158

[3] 34:28

[4] 25:1

[5] al-Bukhaariy (335) na (438) na Muslim (521).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 79-81
  • Imechapishwa: 10/12/2022