Endapo utaulizwa nini maana ya Twaa Haa? Utasema kuwa haina maana katika lugha ya kiarabu. Ni herufi za mkato zinazojulisha kwamba waarabu wameshindwa kuleta mfano wa Qur-aan.

Kuhusu waliosema kuwa Twaa Haa ni miongoni mwa majina ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hana dalili. Ametamka kitu asichokijua. Haikupokelewa kwamba miongoni mwa majina ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Twaa Haa. Endapo atasema: ”Allaah si ndiye ambaye amesema:

طه مَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَىٰ

Twaa Haa. Hatukukuteremshia Qur-aan ili upate mashaka.”?[1]

Nasi tutamuuliza kama Yaa Siyn pia ni jina lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu Allaah amesema:

يس وَالْقُرْآنِ الْحَكِيمِ

”Yaa Siyn. Naapa kwa Qur-aan yenye hekima.”?[2]

Tutamuuliza pia kama Nuun ni jina lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu Allaah amesema:

ن ۚ وَالْقَلَمِ وَمَا يَسْطُرُونَ

”Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo.”?[3]

Tutamuuliza pia kama Aliyf Laam Miym Swaad ni jina lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu Allaah amesema:

المص كِتَابٌ أُنزِلَ إِلَيْكَ

”Alif Laam Miym Swaad. Hiki Kitabu kimeteremshwa kwako.”?[4]

Hakuna yeyote awezaye kusema hivo.

Napenda kuwaambia ndugu zangu kwamba majina yote ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yametokana na maana kuu. Muhammad na Ahmad yanatokana na kusifiwa, al-Haashir mwenye kuwakusanya watu, al-Aaqib ambaye hakuna baada yake Nabii na kadhalika. Majina yote ya Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yametokana na maana kuu na tukufu. Vivyo hivyo majina ya Qur-aan. Hali kadhalika majina ya Mola (´Azza wa Jall). Yote yanatokana na maana tukufu na kuu. Hutopata ndani yake jina lisilokuwa na maana yoyote.

[1] 20:01-02

[2] 36:01-02

[3] 68:01

[4] 07:01-02

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.youtube.com/watch?v=S-TedIc4EDI
  • Imechapishwa: 12/12/2020