91. Tukimbilie wapi wakati wa mizozo na tofauti?

Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

ودعْ عَنْكَ آراءَ الرجالِ وقَوْلَهُمْ

38 – Achana na maono na maneno ya wanaume

فقولُ رسولِ اللهِ أزكَى وأَشْرحُ

     hakika maneno ya Mtume wa Allaah ni takasifu na yanaleta utulivu zaidi

MAELEZO

Haya ni masuala mengine. Ni lazima kati ya wanazuoni kuwepo tofauti katika mambo mbalimbali. Mmoja anasema kitu fulani kuwa ni halali ilihali mwengine anasema kuwa ni haramu. Kati ya wanazuoni kunatokea tofauti katika masuala yanayohusiana na ´Aqiydah, kimatendo na miamala. Ni jambo lisilokuwa na shaka kwamba tofauti hutokea. Haya ndio maumbile ya watu:

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ لَجَعَلَ النَّاسَ أُمَّةً وَاحِدَةً ۖ وَلَا يَزَالُونَ مُخْتَلِفِينَ إِلَّا مَن رَّحِمَ رَبُّكَ

“Kama angetaka Mola wako, basi angejaalia watu wote kuwa ni ummah mmoja. Na hawatoacha kukhitilafiana – isipokuwa yule aliyemrehemu Mola wako.” (11:118-119)

Lakini pamoja na hivyo haijuzu kwetu kuchukua yale maoni tunayoyataka na yanayoafikiana na matashi na matamanio yetu. Tunachotakiwa ni sisi kuchukua yale maoni yaliyosimama juu ya dalili kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wale wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni njia bora na matokeo mazuri zaidi.”  (04:59)

Maneno Yake (Ta´ala):

فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ

“… basi lirudisheni kwa Allaah… “

Katika Kitabu cha Allaah ambacho ni Qur-aan.

وَالرَّسُولِ

“… na Mtume.” (04:59)

Kurejea kwake katika uhai wake (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) na kumuuliza. Kuhusu baada ya kufa kwake mtu arejee katika Sunnah zake. Uwepo wa Sunnah zake ni kana kwamba bado yupo (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Kwa ajili hii ndio maana amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika yeyote atakayeishi muda mrefu katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na walioongozwa baada yangu.”

“Hakika mimi nimekuacheni yale ambayo lau mtashikamana nayo, basi hamtopotea baada yangu: Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu.”[1]

Haijuzu kwetu kuchukua yale maoni tunayoyapenda au yanayoafikiana na matashi au matamanio yetu na tukasema:

“Haya ni yenye nafasi na mepesi kwa watu na kwamba kunatakikana mabadiliko.”

Haya ni maneno batili. Haya ndio maneno yanayosemwa na waandishi na watu wengi wanaofuata matamanio hii leo. Wanasema kuwa tofauti ni rehema. Tunasema kuwa tofauti sio rehema. Kujumuika na umoja ndio rehema. Ama tofauti ni adhabu na shari. Hivyo ndivyo alivyosema ´Abdullaha bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba tofauti ni shari[2]. Tofauti ipo. Lakini haina maana sasa ndio tuseme kuwa ni katika wasaa wa dini. Dini haiko kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni. Dini ni kwa mujibu wa dalili. Amesema (Ta´ala):

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ

“Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume.” (04:59)

Hii ndio mizani ilio kati yetu. Allaah hatukuacha kwenye tofauti wala kwenye maneno na maoni ya fulani na fulani. Bali ametuamrisha kurejea katika mizani: Qur-aan na Sunnah.

Yule ambaye ni katika wanazuoni na anaweza kujua ni maoni yepi yaliyo na nguvu zaidi juu ya mengine, haimfai kwake kuchukua maoni yoyote mpaka ayapime na Qur-aan na Sunnah. Lakini akiwa ni katika watu wasiokuwa wasomi au ndiye sasa ameanza kujifunza elimu, huyu anatakiwa kuwauliza wanazuoni. Amesema (Ta´ala):

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

“Basi waulizeni watu wenye Ukumbusho ikiwa hamjui.” (16:43)

[1] al-Haakim (01/93)

[2] Abu Daawuud (1960), al-Bayhaqiy (03/143) na wengineo

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 192-194
  • Imechapishwa: 13/01/2024