92. Maneno ya kila mmoja yanapimwa kwa Qur-aah na Sunnah

Maimamu wanatahadharisha kuchukua maono yao pasi na kujua dalili.

Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kila mmoja wetu ni mwenye kurudi na anarudiwa isipokuwa mtu mwenye kaburi hili.”

Bi maana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Amesema vilevile:

“Kila ambapo kutakuja mtu bingwa katika kujadili kuliko mwengine tuache yale Jibriyl aliyoteremka nayo kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu ya mijadala ya watu hawa!”

Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inaposihi Hadiyth basi hayo ndio madhehebu yangu.”

Amesema vilevile:

“Maoni yangu yakitofautiana na maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam),  basi yachukueni maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yatupeni maoni yangu kando.”

Amesema tena:

“Waislamu wameafikiana juu ya kwamba yule atayebainikiwa na Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haifai akaiacha kwa ajili ya maneno ya yeyote.”

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ninastaajabishwa na watu wanaojua elimu ya cheni ya wapokezi na usahihi wake halafu wanaenda katika maoni ya Sufyaan ilihali Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Na watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije ikawapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.” (24:63)

Unajua ni ipi fitina? Fitina ni shirki. Huenda ataporudisha baadhi ya maneno yake kukaingia ndani ya moyo wake kitu katika upindaji akaangamia.”

Hakuna maneno ya yeyote yanayosimama pamoja na maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni wajibu juu yetu wakati wa tofauti turejee katika mizani. Hii ni huruma ya Allaah kwetu ya kwamba hakutuacha juu ya tofauti na maoni ya watu. Kinyume chake ametuamrisha kuyapima maoni mbalimbali na Qur-aan na Sunnah. Hili linawahusu wanazuoni. Kuhusu wasiokuwa wasomi wanachotakiwa ni kuwauliza wanazuoni:

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

“Basi waulizeni watu wenye Ukumbusho ikiwa hamjui.” (16:43)

Amuulize yule mwanachuoni anayeamini elimu na dini yake na atendee kazi maneno yake. Kwa ajili hii ndio maana wanasema:

“Madhehebu ya asiye msomi ni madhehebu ya yule anayemjibu.”

Hiki ndicho kigezo katika masuala haya.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 194-195
  • Imechapishwa: 13/01/2024