90. Muumini mwenye nguvu anapendeza zaidi kwa Allaah kuliko muumini dhaifu

Murji-ah wanapinga na kusema haizidi na wala haipungui. Wanasema kuwa imani ni kitu kiko moyoni na ni kitu kimoja tu. Hawaoni kuwa watu wanashindana katika imani. Wanaonelea kuwa imani ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) ni sawa na imani ya mtenda dhambi mkubwa kabisa. Hii ni ´Aqiydah batili. Baadhi ya waumini imani zao ni zenye nguvu zaidi kuliko wengine. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muumini mwenye nguvu ni bora na anapendwa zaidi na Allaah kuliko muumini dhaifu – na kwa wote wawili kuna kheri.”[1]

Inahusiana na nguvu za kiimani, za kimwili na za kimatendo.

Imani inazidi na kupungua bila ya shaka. Maasi yanaipunguza imani ilihali mambo ya utiifu yanaiongeza. Hii ndio maana ya imani kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Sema kuwa imani ni maneno…”

Bi maana kutamka kwa ulimi.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“… na nia… “

Bi maana kuamini kwa moyo.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“.. na kitendo… “

Matendo ya viungo.

Kwa hivyo imani ni maneno, kuamini na matendo. Haya ndiyo yenye kufahamishwa na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama ilivyo katika Hadiyth ya tanzu za imani na nyenginezo.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inapungua kwa maasi wakati fulani… “

Hii ni Radd kwa Murji-ah wanaosema kuwa imani haizidi na wala haipungui. Wanasema kuwa ni kitu kimoja na watu wake katika msingi wake wanalingana. Hii ni ´Aqiydah batili. Ukweli wa mambo ni kuwa imani inazidi kwa utiifu na inashuka kwa kufanya maasi.

[1] Muslim (2667)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 191
  • Imechapishwa: 13/01/2024