Talaka ni mikononi mwa mwanaume na si mwanamke

Swali: Hii leo, mbali na Makkah na al-Madiynah, baadhi ya miji ya Kiislamu imetoa baadhi ya fatwa zinazohusiana na dini ikiwa ni pamoja vilevile na kwamba talaka iko mikononi mwa mwanamke. Una nasaha gani juu ya hilo?

Jibu: Nasaha zangu juu ya hili ni kwamba yule aliyesema kuwa talaka iko mikononi mwa mwanamke si jambo la sawa na si sahihi. Ni jambo linalopingana na Qur-aan tukufu. Allaah (´Azza wa Jall) amesema ndani ya Qur-aan:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا

“Enyi walioamini! Mnapofunga ndoa na waumini wa kike kisha mkawataliki kabla ya kuwajamii, basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu.”[1]

وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ إِلَّا أَن يَعْفُونَ أَوْ يَعْفُوَ الَّذِي بِيَدِهِ عُقْدَةُ النِّكَاحِ

“Mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia kwao mahari, basi wapeni nusu ya hayo mliyobainisha isipokuwa wakisamehe au asamehe yule ambaye mkataba wa ndoa uko mikononi mwake.”[2]

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ

“Ee Nabii!  Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa twahara zao na hesabuni vyema eda.”[3]

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ

“Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah amefadhilisha baadhi yao juu ya wengine na pia kwa yale wanayotoa katika mali zao.”[4]

Imekuja katika Hadiyth ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Talaka ni kwa yule aliyeshika muundi.”

Nadhani kwamba jambo hili linapingana na maafikiano ya waislamu kwamba eti talaka iwe mikononi mwa mwanamke.

Upande wa akili mwanamke ni mwenye hisia za haraka na akili pungufu. Iwapo atamuona mwanaume ambaye ni mrembo kuliko mume wake basi papohapo ataenda kwa mume wake na kumwambia kuwa amemtaliki mara tatu pasi na rejea[5]. Kwa sababu mwanamke huyu anamtarajia huyu mwanaume mrembo. Lau mume wake atamfanyia kosa dogo basi atamtaliki talaka tatu. Hili ni jambo geni. Huku ni kupindukia uhakika wa mambo.

Ni kweli kwamba ikiwa kuna masharti ambayo alimuwekea mume na asiyatimize, basi na haki ya kufuta ndoa (الفسخ). Hatuiti kuwa ni talaka. Tunaita kuwa ni kufuta kwa ndoa na haihesabiki kuwa ni talaka na wala haipunguzi idadi ya talaka.

[1] 33:49

[2] 02:237

[3] 65:01

[4] 04:34

[5] Tazama https://firqatunnajia.com/hekima-ya-allaah-kutompa-mwanamke-akamiliki-talaka/

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (71) http://binothaimeen.net/content/1652
  • Imechapishwa: 12/08/2020