Swalah ya sunnah moja kwa moja baada ya ´Aswr

3173- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Umefanya vizuri Ibn-ul-Khattwaab.”

Ameipokea Ahmad: Muhammad bin Ja´far ametuhadithia: Shu´bah ametuhadithia, kutoka kwa al-Azraq bin Qays, kutoka kwa ´Abdullaah bin Rabaah, kutoka kwa mmoja katika Mswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumaliza kuswali ´Aswr, alisimama bwana mmoja kuswali. Wakati ´Umar alipomuona akachukua nguo au kanzu yake na akasema: “Keti chini. Hakika si vyenginevyo kilichowaangamiza watu wa Kitabu ni kwamba hakukuwa na kipambanuzi kati ya swalah zao.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Umefanya vizuri Ibn-ul-Khattwaab.”

Abu Ya´laa pia ameipokea katika “al-Musnad” yake. Cheni ya wapokezi ni Swahiyh na wapokezi wote ni waaminifu kwa mujibu wa sharti za Muslim. Isipokuwa Swahabah ambaye hakutajwa jina, lakini hata hivyo haidhuru, kwa sababu Maswahabah wote ni waadilifu.

Hadiyth inafahamisha kufaa kuswali swalah za sunnah baada ya ´Aswr. Kutokana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumkubalia bwana huyo aliyekuwa anataka kuswali baada ya ´Aswr, kisha kukubaliwa na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh).  Hata hivyo ´Umar alichomkemea ni yeye kuacha kipambanuzi, jambo ambalo alikubaliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo ikafahamisha kuwa inafaa kuswali swalah ya sunnah baada ya ´Aswr pasi na kuunganisha. Kinachojulisha juu ya kufaa kwake ni kwamba yeye mwenyewe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali baada ya ´Aswr. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haachi Rak´ah mbili baada ya Fajr na Rak´ah mbili baada ya ´Aswr.”

Kitendo hicho kimethibiti kutoka kwa Salaf wengi (Radhiya Allaahu ´anhum).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (7/1/522)
  • Imechapishwa: 12/08/2020