Tafsiri ya Hadiyth “Mwenye kuomba kwa jina la Allaah basi atoe”

Swali: Ni ipi hukumu ya mwenye kuombwa kwa jina la Allaah na asiitikie? Ni ipi hukumu ya mwenye kuombwa kwa jina la Allaah na asifanye jambo hilo?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuombwa kwa jina la Allaah basi atoe.”[1]

Isipokuwa tu ikiwa kama hana haki ya kile anachoomba. Kwa mfano akasema “Nakuomba kwa jina la Allaah unipe katika zakaah” ilihali sio katika wenye kuiistahiki. Katika hali hiyo hatopewa. Lakini hata hivyo akiomba kitu kilicho na utata kama kuomba kutoka katika nyumba ya mali ya waislamu au akaomba apewe na kusema kuwa ni fakiri anatakiwa kupewa:

“Mwenye kuombwa kwa jina la Allaah basi atoe.”

Lakini haitakiwi kuomba kwa jina la Allaah. Haifai kuwatia watu uzito. Kwa ajili hii Malaika yule aliyemwendea mwenye ukoma, kipofu na mwenye kipara alisema kuwaambia:

“Ninakuomba kwa jina la Yule aliyewapa kadhaa na kadhaa.”

Aliwaomba kwa jina la Allaah. Makusudio ni kuwa mtu akiomba kwa jina la Allaah kitu muhimu basi apewe akiwa anastahiki. Ama akiwa hastahiki hapewi na wala yeye hatakiwi kuomba kwa jina la Allaah. Kama akisema “Ninakuombeni kwa jina la Allaah mnipe katika zakaah” na wakati huo huo sio katika wale wenye kuistahiki hatakiwi kupewa zakaah. Kwa kuwa sio katika wale wenye kuiistahiki. Mfano mwingine akasema “Ninawaombeni kwa jina la Allaah mnipe mali yenu yote mlionayo na wala msibaki na kitu”. Katika hali hii hatakiwi kupewa.

[1] Abu Daawuud (1672) na an-Nasaa´iy (2567).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 119
  • Imechapishwa: 09/01/2017