Swali: Kuna ambaye anafunga na kutekeleza baadhi ya ´ibaadah lakini haswali. Je, inakubaliwa swawm na ´ibaadah zake?

Jibu: Maoni sahihi ni kwamba mwenye kuacha swalah anakufuru ukafiri mkubwa. Hivyo haisihi swawm wala ´ibaadah zake nyenginezo mpaka atubu kwa Allaah (Subhaanah). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda.”[1]

Zipo Aayah na Hadiyth nyenginezo zilizokuja zikiwa na maana kama hiyo.

Kuna kikosi kingine cha wanazuoni waliosema kuwa hakufuru ukafiri mkubwa na funga na ´ibaadah zake nyenginezo hazibatiliki muda wa kuwa ni mwenye kukubali kuwa ni wajibu. Ameacha swalah kutokana na uzembe na uvivu. Lakini maoni sahihi ni hayo ya kwanza; ni kwamba anakufuru ukafiri mkubwa akiwa ni mwenye kukubali uwajibu wake. Msimamo huo ni ktuokana na dalili nyingi kukiwemo maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha swalah.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi, yule atakayeiacha amekufuru.”

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa nne wa Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Buraydah bin al-Huswayb al-Aslamiy (Radhiya Allaahu ´anh).

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amelizungumzia hilo kwa kina katika kitabu cha kujitegemea kuhusu hukumu ya swalah na kuiacha. Ni kitabu chenye faida ambacho ni vizuri kukirejea na kufaidika nacho.

[1] 06:88

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/267)
  • Imechapishwa: 06/10/2021