´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 10: Ni ipi hukumu ya matendo ya waja?

Jibu: Matendo ya waja yote, ya utiifu na maasi, yanaingia katika uumbaji wa Allaah, mipango na makadirio.

Hata hivyo wao ndio wenye kuyafanya. Allaah hakuwalazimisha nayo. Wanayafanya kwa kutaka kwao na kwa uwezo wao.

Ni matendo yao kihakika. Wanasifiwa na kulipwa kwayo na kuadhibiwa kwayo.

Matendo ni uumbaji wa Allaah kihakika. Allaah amewaumba, akaumba matakwa yao, uwezo wao na yote yanayopitika kwa hilo.

Tunaamini maandiko yote ya Qur-aan na Sunnah yenye kuthibitisha ueneaji wa uumbaji na uwezo wa Allaah juu ya kila kilichopo na kupitika.

Hali kadhalika tunaamini maandiko yote ya Qur-aan na Sunnah yenye kuthibitisha kuwa ni waja ndio wenye kufanya matendo mazuri na mabaya na kwamba wao wenyewe ndio wenye kuchagua matendo yao. Allaah ameumba nguvu na matakwa yao. Mambo hayo mawili ndio sababu ya kupatikana matendo yao na maneno yao. Yule mwenye kuumba sababu anaumba pia chenye kusababishwa. Allaah ni mkubwa na mwadilifu kuwatenza nguvu matendo.

MAELEZO

Allaah ndiye ameumba na kufanya kupatikana kwa kheri na shari, imani na ukafiri, utiifu na maasi. Pamoja na hivo waja ndio wameyafanya na kuyachuma. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye ambaye kawaumba waja na uwezo na matakwa yao. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameeleza kuwa Ibraahiym (´alayhis-Salaam) amesema:

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah amekuumbeni pamoja na vile mnavovifanya.”[1]

Matendo ya waja yamekadiriwa na Allaah. Allaah ameyaandika kwenye Ubao unaohifadhi. Allaah amekwishawaandika waja Wake wenye furaha na waja wenye kula maangamivu pamoja na mwenye kutii na mwenye kuasi.

Qadar ni siri ya Allaah. Hakuna yeyote awezaye kuifichua. Ahl-us-Sunnah wanaogopa kuingia sana kwa undani. Hivo ni kwa kuwaigiliza wema wao waliotangulia.

Katika Qur-aan kuna viashirio vinavyojulisha kwamba Allaah (´Azza wa Jall) anawakosesha nusura watu fulani na hivyo akawakadiria maangamivu. Akawafanya wao wenyewe kujichagulia maangamivu na njia zake zenye kuyasababisha. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَنُقَلِّبُ أَفْئِدَتَهُمْ وَأَبْصَارَهُمْ كَمَا لَمْ يُؤْمِنُوا بِهِ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَنَذَرُهُمْ فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ

“Tunazigeuza nyoyo zao na macho yao kama ambavo hawakuiamini mara ya kwanza na tunawaacha katika kuchupa kwao mipaka wakitangatanga.”[2]

فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ

“Pindi walipopotoka, basi Allaah akazipotosha nyoyo zao.”[3]

إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ

“Hakika Allaah hayabadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe kwanza wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao.”[4]

Aayah hizi zinafahamisha kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) huwaadhibu baadhi ya waja Wake kwa sababu ya kuupa kwao mgongo uongofu Wake na kujiweka nao mbali.

Jengine ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametueleza kuwa hawadhulumu waja Wake lakini waja wao wenyewe ndio wenye kuzidhulumu nafsi zao. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ

“Hatukuwadhulumu, lakini walikuwa wanajidhulumu nafsi zao wenyewe.”[5]

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ

“Hakika Allaah hadhulumu uzito wa atomu.”[6]

مَّنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا ۗ وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ

”Yeyote atakayetenda mema, basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na yeyote atakayefanya maovu, basi ni dhidi yake; na Mola wako si Mwenye kudhulumu kamwe waja.”[7]

 Allaah anamwongoza amtakaye kwa fadhilah Zake na anampotosha amtakaye kwa uadilifu Wake. Amesema (Ta´ala):

لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ

“Haulizwi [Allaah] kwa yale anayoyafanya, lakini wao wataulizwa.”[8]

Waliozungumzia kuhusu Qadar ni makundi mawili:

1 – Jabriyyah. Wanasema kuwa Allaah amewatenza nguvu watu juu ya maangamivu na akawaadhibu kwa hayo. Hawa wamemnasibishia Allaah dhuluma. Allaah (Subhaanahu wa Ta´a) amejiharamishia dhuluma juu ya nafsi Yake na akaifanya kuwa haramu kati yetu. Imekuja katika Hadiyth al-Qudsiy:

“Ee waja Wangu! Hakika mimi nimejiharamishia dhuluma juu ya nafsi Yangu na kuifanya kati yenu kuwa haramu. Hivyo msidhulumiane.”[9]

Maneno ya watu hawa yanapelekea kwamba Allaah amewatenza nguvu watu juu ya ukafiri na maasi kisha akawaadhibu kwayo. Hivyo kuwaadhibu ni kuwadhulumu. Nadharia hii ni mbaya zaidi kuliko yale waliyoyaepuka.

2 – Qadariyyah. Wanasema kuwa kufuru na maasi ni matendo ya waja na hayakukadiriwa na Allaah (´Azza wa Jall). Watu hawa kitu cha kwanza wamethibitisha waumbaji wawili. Wanaona kuwa Allaah ndiye kaumba utiifu na imani na mja ndiye mwenye kuumba kufuru na maasi. Kwa ajili hiyo wakafananishwa na waabudia moto. Kitu cha pili ni kwamba wanaposema kuwa kufuru haikukadiriwa na Allaah (´Azza wa Jall) hiyo ina maana kwamba katika ulimwengu kunatokea yale ambayo hayakukadiriwa wala kutakwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hayo yanapelekea kuwa Allaah ni mwenye kushindwa.

Kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, wanasema kwamba kheri na shari, utiifu na maasi, kufuru na imani, vyote hivo vinatokana na Qadar ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Waja wanafanya matendo kwa kutaka kwao wenyewe. Wao wenyewe ndio wenye kujichagulia ukafiri juu ya imani, maasi juu ya utiifu, upotofu juu ya uongofu. Hawana hoja yoyote mbele ya Allaah. Anawahukumu kwa hekima kubwa. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hii ndio ´Aqiydah ya haki waliokuwa nayo Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Viumbe wote ni waja wa Allaah. Iwapo angeliwaadhibu wote basi angelifanya hivo pasi na kuwadhulumu. Waja ndio wameyafanya matendo hayo kwa kutaka kwao wenyewe. Yule mwenye kufanya mazuri, atalipwa thawabu na Allaah. Yule mwenye kufanya maasi, Allaah atamuadhibu akitaka na akitaka atamsamehe. Vivyo hivyo imani na ukafiri. Yule mwenye kufa juu ya ukafiri ni lazima aadhibiwe na Allaah Motoni. Yule mwenye kufa hali ya kuwa ni muislamu basi hapana shaka kuwa ataingia Peponi.

Muislamu anatakiwa siku zote kumuomba Allaah uimara juu ya nafsi yake na amwongoze. Ndio maana Allaah ameweka katika Shari´ah kusoma al-Faatihah na ndani yake mna:

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ

“Tuongoze njia iliyonyooka.”[10]

Imesuniwa kusoma hivo katika kila Rak´ah ili mja awe mwenye kumuomba Allaah (´Azza wa Jall) amwongoze katika njia ilionyooka na amlinde kutokamana na njia zilizopotea. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) daima alikuwa ni mwenye kuomba kwa kusema:

“Ee mwenye kuzipindua nyoyo! Uthibitishe moyo wangu juu ya dini yako.”[11]

Hivyo basi na sisi tunapaswa kuomba hivo kwa wingi.

[1] 37:96

[2] 06:110

[3] 61:05

[4] 13:11

[5] 16:118

[6] 04:40

[7] 41:46

[8] 21:23

[9] Muslim (2477).

[10] 01:06

[11] at-Tirmidhiy (3522). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwilaal-ul-Jannah” (223).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 61-65
  • Imechapishwa: 06/10/2021