Anahalalisha ya haramu kutokana na ujinga

Swali: Kuna kigezo kipi cha mtu kuwa kafiri endapo atahalalisha?

Jibu: Kuhalalisha maana yake ni pale atapoonelea kuwa halali kile alichoharamisha Allaah. Kuhusu uhalalishaji wa kimatendo, basi mtu anatakiwa kuangalia kama kile kitendo chenyewe ni ukafiri. Ikiwa ni kitendo cha kufuru, basi ni kafiri kupitia kitendo hicho alichofanya. Kwa mfano mtu anakula ribaa pasi na kuona kuwa ni halali. Lakini hata hivo ni mwenye kuendelea daima juu yake. Mtu huyu hakufuru kwa sababu haonelei kuwa ni halali. Lakini endapo atasema kuwa ribaa ni halali na anakusudia ile ribaa aliyoharamisha Allaah, basi anakufuru kwa sababu ni mwenye kumkadhibisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa hivyo kuna aina mbili za uhalalishaji; uhalalishaji wa kimatendo na uhalalishaji unaokuwa ndani ya moyo. Kuhusu uhalalishaji wa kimatendo, inatakiwa kuangalia kitendo chenyewe kama ni cha ukafiri au sio cha ukafiri. Kama inavotambulika mlaji ribaa hakufuru. Lakini dhambi hiyo ni miongoni mwa madhambi makubwa. Iwapo mtu atasujudia sanamu, huyu anakufuru. Kwa nini? Kwa sababu kitendo chenyewe kama chenyewe ni ukafiri. Hiki ndio kigezo.

Ni lazima kuwepo sharti nyingine. Mtu huyu mhalalishaji asiwe ni mwenye kupewa udhuru kutokana na ujinga wake. Akiwa ni mwenye kupewa udhuru kutokana na ujinga wake, hakufuru. Kwa mfano mtu ndio punde ameingia ndnai ya Uislamu na hajui kuwa pombe ni haramu. Mtu huyu hata kama atahalalisha hakufuru mpaka kwanza afunzwe kuwa ni haramu. Akiendelea kusema kuwa ni halali baada ya kujifunza, anakufuru.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (50 B)
  • Imechapishwa: 06/10/2021