Swali: Ni ipi hukumu ya swalah zilizonipita? Je, nalazimika kuzilipa au nifanye kitu gani? Kwa sababu nimesikia Hadiyth kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayepitwa na swalah na asiidhibiti, basi aiswali mwishoni mwa ijumaa ya Ramadhaan na aswali Rak´ah nne na amtake Allaah msamaha baada yake.”

Je, haya ni sahihi?

Jibu: Hadiyth hii si sahihi na wala haina msingi. Lakini ni lazima kwako kuilipa. Mtu akiacha swalah kwa kusahau au kupitiwa na usingizi, basi anatakiwa kuilipa. Ama akiwa ameiacha kwa makusudi pasi na kuelewa makosa, hatoilipa. Kwa sababu kuacha swalah ni ukafiri mkubwa ijapo hatopinga uwajibu wake kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Lakini akiacha swalah hali ya kupinga uwajibu wake basi anakufuru kwa maafikiano ya wanazuoni wote. Ama akiwa anakubali uwajibu wake na anatambua kwamba ni faradhi juu yake, hata hivyo akaiacha kwa sababu ya kuzembea na kuhisi uvivu, huyu hukumu yake wanazuoni wametofautiana.

Maoni sahihi juu ya masuala haya ni kwamba amekufuru kufuru kubwa na hatolipa. Ni lazima kwake kutubu juu ya yale yaliyotangulia na kunyooka kuiteleza katika mustakabali.

Kuhusu mwenye kuiacha kutokana na maradhi, kusahau au kupitiwa na usingizi basi huyu ndiye anatakiwa kuilipa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kulala akapitiwa na usingizi au akaisahau basi aiswali wakati atakapoikumbuka. Hana kafara nyingine isipokuwa hiyo.”

Amesema (Ta´ala):

قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُم مَّا قَدْ سَلَفَ

“Waambie wale waliokufuru kwamba wakikoma watasamehewa yaliyotangulia.”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tawbah inafuta yaliyokuwa kabla yake na Uislamu unafuta yaliyokuwa kabla yake.”

Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba  amesema:

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi, yule atakayeiacha amekufuru.”

Amesema pia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kichwa cha mambo ni Uislamu, nguzo yake ni swalah na jihaad katika njia ya Allaah ndio nundu yake ya juu.”

Vilevile amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Baina ya mtu na shirki na kufuru ni kuacha swalah.”

Ameipokea Muslim (Rahimahu Allaah) katika “as-Swahiyh” yake.

Dalili hizi na nyenginezo zilizokuja zikiwa na maana yake zinajulisha ukafiri wa mwenye kuacha swalah kwa makusudi kwa kuzembea na kwa kuhisi uvivu na si kwa sababu ya kupitiwa na usingizi au ugonjwa unaomjuzishia kuchelewesha au kwa kusahau. Mwenye kusahau, mgonjwa na mgonjwa ambaye inafaa kwake kuchelewesha wanatakiwa kulipa. Ama mwenye kukusudia na mwenye kuchukulia wepesi haifai kwao kulipa. Ni lazima kwao kutubu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kama tulivyotangulia kusema.

[1] 08:38

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/315)
  • Imechapishwa: 04/10/2021