´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 9: Waumini wamegawanyika daraja ngapi na ni zipi?

Jibu: Waumini wamegawanyika daraja tatu:

1 – Waliotangulia katika mambo ya kheri. Ni wale wenye kufanya yale ya wajibu na yaliyopendekezwa na wakajiepusha na yale ya haramu na yenye kuchukiza.

2 – Wa kati na kati. Ni wale wenye kufanya yale ya wajibu na kujiepusha na yaliyoharamishwa.

3 – Aliyejidhulumu nafsi. Ni wale wenye kuchanganya matendo mazuri na mabaya.

MAELEZO

Vigawanyo hivi vimetajwa katika maneno ya Allaah (Ta´ala):

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ

“Kisha Tukawarithisha Kitabu wale tuliowateuwa miongoni mwa waja Wetu. Basi miongoni mwao ni aliyedhulumu nafsi yake na miongoni mwao aliyekuwa kati na kati na miongoni mwao aliyetangulia kwa mambo ya kheri kwa idhini ya Allaah – hiyo ndio fadhilah kubwa.”[1]

Namna hii ndivo wanavyogawanywa wale waliowaitikia Mitume. Ni waislamu kwa mpangilio huu:

1 – Waliotangulia katika mambo ya kheri. Ni wale wenye kufanya yale ya wajibu na yaliyopendekezwa na wakajiepusha na yale ya haramu na yenye kuchukiza.

2 – Wa kati na kati. Ni wale wenye kufanya yale ya wajibu na kujiepusha na yaliyoharamishwa.

3 – Waliojidhulumu nafsi zao. Ni wale wenye kuchanganya matendo mazuri na mabaya. Allaah (Subhaanah) amesema juu yao:

وَآخَرُونَ اعْتَرَفُوا بِذُنُوبِهِمْ خَلَطُوا عَمَلًا صَالِحًا وَآخَرَ سَيِّئًا عَسَى اللَّـهُ أَن يَتُوبَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Na wengineo wametambua madhambi yao – wamechanganya matendo mema na mengine maovu – pengine Allaah akawasamehe. Hakika Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[2]

Wale waliotangulia katika mambo ya kheri watapata ngazi za juu zaidi Peponi baada ya Mitume. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ أُولَـٰئِكَ الْمُقَرَّبُونَ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ثُلَّةٌ مِّنَ الْأَوَّلِينَ وَقَلِيلٌ مِّنَ الْآخِرِينَ عَلَىٰ سُرُرٍ مَّوْضُونَةٍ مُّتَّكِئِينَ عَلَيْهَا مُتَقَابِلِينَ

“Waliotangulia mbele – watatangulia mbele. Hao ndio watakaokurubishwa katika mabustani yenye neema. Kundi kubwa katika wa mwanzo; na wachache katika wa mwishoni. Watakuwa juu ya makochi ya fakhari yaliyotonewa. Wakiegemea juu yake wakielekeana.”[3]

Kisha baada ya hapo akataja watu wa upande wa kuume, nao ni wale wa kati na kati, kwa kusema:

وَأَصْحَابُ الْيَمِينِ مَا أَصْحَابُ الْيَمِينِ فِي سِدْرٍ مَّخْضُودٍ وَطَلْحٍ مَّنضُودٍ  وَظِلٍّ مَّمْدُودٍ

“Na watu wa kuliani – je, kina nani watu wa kuliani? Watakuwa miongoni mwa mikunazi isiyokuwa na miba na migomba iliyopangiliwa na kivuli kilichotandazwa.”[4]

Amewanyamazia wale waliojidhulumu nafsi zao kwa sababu wako khatarini. Hukumu ndani ya Qur-aan mara nyingi inakuwa namna hii. Waumini hutajwa kwa uzuri wa matendo yao na wakatajwa wale wa chini yao ambao ni wale wa kati na kati. Mara nyingi hunyamaziwa wale waliojidhulumu nafsi zao. Nao ni wale wenye kutenda madhambi makubwa. Mara kadhaa hutajwa wale wenye kujiepusha na madhambi makubwa na kukatajwa malipo gani yanayowasubiri.

Kuhusu wale wenye kufanya madhambi makubwa kama kwa mfano utovu wa nidhamu kwa wazazi wawili, kukata udugu, kuchukua mali za watu pasi na haki na kuzikiuka heshima za watu, Allaah huwataja kwa ubaya. Sunnah imebainisha kuwa watu aina hii wataadhibiwa Motoni kwa kiasi cha madhambi yao. Kisha baada ya hapo watasalimishwa na adhabu ya Moto na kuondoshwa ndani yake kiasi cha kwamba hatobaki ndani yake yeyote yule aliye na imani moyoni mwake sawa na mduduchungu.

Allaah (´Azza wa Jall) amewagawanya viumbe mafungu matatu katika Suurah “al-Waaqi´ah”. Wale waliowatikia Mitume amegawanya makundi mawili; wale waliotangulia na watu wa upande wa kuume. Fungu la tatu ni watu wa upande wa kushoto. Watu hao ni wale waliokufa juu ya ukafiri pasi na kujali ukafiri wao. Haijalishi kitu ukafiri wao ilikuwa ukanamungu, kama mfano wa kumkanusha Muumba au kufufuliwa, ukafiri wa ukhurafi na masanamu, kama mfano wa wale wanaoabudiwa pamoja na Allaah waungu wengine na wakomunisti ambao wanafanya shirki kubwa, ukafiri wa kuwa na shaka, kama wale wenye unafiki wa kiimani. Watu wote hawa ni wenye kudumishwa Motoni milele. Allaah amewakusanya wote pale aliposema:

وَأَصْحَابُ الشِّمَالِ مَا أَصْحَابُ الشِّمَالِ فِي سَمُومٍ وَحَمِيمٍ وَظِلٍّ مِّن يَحْمُومٍ  لَّا بَارِدٍ وَلَا كَرِيمٍ

”Na watu wa kushotoni – je, ni kina nani watu wa kushotoni? Watakuwa kwenye Moto ubabuao na maji yanayochemka na kivuli cha moshi mweusi mnene wa joto kali mno. Si cha kuburudisha wala kustarehesha.”[5]

Mwishoni mwa Suurah amewagawanya mafungu matatu: mafungu mawili katika wao wamewaitikia Mitume na fungu la tatu ni makafiri pasi na kujali ukafiri wao. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

فَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُقَرَّبِينَ فَرَوْحٌ وَرَيْحَانٌ وَجَنَّتُ نَعِيمٍ وَأَمَّا إِن كَانَ مِنْ أَصْحَابِ الْيَمِينِ فَسَلَامٌ لَّكَ مِنْ أَصْحَابِ الْيَمِينِ وَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُكَذِّبِينَ الضَّالِّينَ فَنُزُلٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَتَصْلِيَةُ جَحِيمٍ إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ حَقُّ الْيَقِينِ فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ

“Basi akiwa miongoni mwa waliokurubishwa [kwa Allaah], basi [atapata] mapumziko ya raha na manukato na Pepo ya neema. Na kama akiwa miongoni mwa watu wa kuliani, basi [atasalimiwa kwa kuambiwa] “Amani juu yako uliye katika watu kuliani!”. Na kama akiwa miongoni mwa wakadhibishaji waliopotoka, basi mapokezi yake ni maji ya Moto yachemkayo na kuchomwa na Moto uwakao vikali mno. Hakika hii bila shaka ni haki yenye yakini. Basi tukuza kwa jina la Mola wako Mtukufu, Mkuu kabisa.”[6]

Namna hii ndivo Allaah amewaganya waja Wake. Tunamuomba Allaah atujaalie kuwa miongoni mwa wale wenye kumtii na kumwamini.

[1] 35:32

[2] 9:102

[3] 56:10-16

[4] 56:27-30

[5] 56:41-44

[6] 56:88-96

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 52-55
  • Imechapishwa: 04/10/2021