Swalah iliyompita mtu anatakiwa kuiswali papo hapo

396 – Abu Juhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba alikuwa katika safari yake ambayo walipitikiwa na usingizi wakalala mpaka kuchomoza kwa jua. Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika nyinyi mlikuwa wafu ambapo Allaah akawarudishia roho zenu. Yule mwenye kupitikiwa na usingizi kwa swalah basi aiswali anapoamka na yule mwenye kusahau swalah basi aiswali atapokumbuka.”

Ameipokea Abu Ya´laa katika ”al-Musnad” (1/58) na at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (22/107) kupitia kwa ´Abdul-Jabbaar bin al-´Abbaas al-Hamadaaniy, kutoka kwa ´Awn bin Abiy Juhayfah, kutoka kwa baba yake.

Cheni ya wapokezi ni nzuri.

Maana ya Hadiyth imepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim na wengineo kupitia kwa Anas na wengineo kwa ziada inayosema:

“Haina kafara nyingine isipokuwa hiyo.”

Hadiyth inajulisha kwamba yule mwenye kupitikiwa na usingizi au mwenye kusahau swalah bado inamuwajibikia kuharakisha kuiswali pale tu atakapoamka na atapoikumbuka. Ziada ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh) inafahamisha kwamba hiyo ndio kafara yake. Vinginevyo hakuna kitendo kingine kinachoweza kuifuta [hiyo dhambi], isipokuwa labda tawbah ya kweli.

Inafahamisha pia kwamba swalah ambayo mtu anaichelewesha kwa makusudi haifidiwi kwa kuiswali baada ya wakati wake. Kwa sababu hana udhuru. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا

“Kwani hakika swalah kwa waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalum.”[1]

Hali si hivyo kwa mtu ambaye amepitikiwa na usingizi au amesahau. Huyu ni mwenye kupewa udhuru kwa andiko la Hadiyth. Kwa ajili hiyo ndio maana kafara yake ikawa pale tu atakapoikumbuka. Huoni kwamba hata huyu ambaye amepewa udhuru asipoharakisha kuiswali papo hapo anapokumbuka basi na yeye pia hana kafara baada ya hapo? Kwa sababu amepoteza wakati ambao Allaah amemuwekea katika Shari´ah kuiswali swalah iliyompita.

[1] 04:103

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naasir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (1/2/752-753)
  • Imechapishwa: 20/08/2020