Sunnah ya Fajr inaswaliwa baada ya kuingia wakati wa Fajr

Swali: Niliingia msikitini katika swalah ya Subh na nikaswali Rak´ah mbili. Wakati niliposimama katika Rak´ah ya pili akasimama muadhini kuadhini kwa ajili ya swalah. Swalah hiyo nilikuwa nimenuia kuwa ni Sunnah ya Subh kwa sababu nilikuwa nimetoka nyumbani na kusikia kunaadhiniwa katika baadhi ya misikiti. Wakati nilipomaliza kuswali nikaketi chini kusoma Qur-aan. Mtu mmoja pambizoni mwangu akanambia nisimame niswali Sunnah ya Subh ambapo nikamjibu kwamba nimeshaswali. Akasema kwamba haifai kufanya hivo isipokuwa natakiwa kuswali mara nyingine kwa sababu muadhini ameadhini ilihali mimi niko naswali. Nataraji kufaidishwa juu ya hilo.

Jibu: Ikiwa muadhini aliyeadhini wakati uko unaswali Sunnah ya Fajr alichelewesha adhaana na kitendo chako kilifanywa baada ya kuchomoza kwa alfajiri, basi umekwishatekeleza Sunnah na inakutosha. Katika hali hiyo hapana haja ya kuirudi. Lakini ikiwa una mashaka juu ya hilo na hujui kama yule muadhini ambaye ameadhini kipindi uko unaswali adhaana yake ni baada ya asubuhi au wakati wa kuchomoza kwa alfajiri, basi salama na bora zaidi kwako urudi kuswali Rak´ah mbili ili uwe na yakini kuwa umeswali baada ya kuchomoza kwa alfajiri.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/369)
  • Imechapishwa: 07/11/2021