Sujuud ya kisomo kwa asiyekuwa na twahara na hakuelekea Qiblah

Swali: Je, nusujudu ikiwa nasoma Qur-aan tukufu pasi na kuelekea Qiblah na nikapitia Aayah ilio na Sujuud? Je, Sujuud ya kisomo inashurutisha mtu awe na twahara? Je, nisujudu hali ya kuwa juu ya kiti nikiwa nasoma Qur-aan tukufu na mimi ni mwenye kusafiri kwa gari au ndege na nikapitia nikapitia Aayah ilio na Sujuud? Nifanyeje ikiwa nitaipitia ilihali nimeketi juu ya kiti ofisini au nyumbani?

Jibu: Sunnah kwa ambaye atapitia Aayah ya sijda wakati yuko anasoma asujudu hali ya kumwigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati mwingine alikuwa anasoma kati ya Maswahabah zake. Anapopita kwenye Aayah ilio na sijda basi anasujudu nao wanasujudu pamoja naye.

Ni Sunnah kuelekea Qiblah ikiwa ni wepesi kufanya hivo. Sujuud ya kisomo sio kama Sujuud ya swalah. Bali  ni kumnyenyekea Allaah na kumwigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo haishurutishi zile sharti za swalah. Hakuna dalili ya hayo. Jengine ni kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisoma Qur-aan katika vikao vyake kati ya Maswahabah zake. Akifikia Aayah ya Sujuud basi anasujudu nao wanasujudu pamoja naye. Hakuwahi kuwaambia kwamba asisujudu isipokuwa yule ambaye yuko na twahara. Vikao hukusanya wale wenye twahara na wale wasiokuwa na twahara. Kwa hiyo ingelikuwa twahara ni sharti basi angewazindua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya hilo. Kwa sababu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mfaswaha zaidi wa watu na isitoshe Allaah amemwamrisha afikishe. Lau twahara ingelikuwa ni sharti katika Sujuud ya kisomo basi angewafikishia jambo hilo (Radhiya Allaahu ´anhum). Angeliwafikishia basi wangeyanukuu hayo kwa wale waliokuja baada yao kama walivyomnukulia historia na maisha yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kama msomaji atakiwa juu ya ndege, gari, meli au juu ya kipando cha safari, basi asujudu upande kule kinaelekea. Hivo ndivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya katika safari zake katika swalah zilizopendekezwa. Ikiwa ni wepesi kwake kuelekea Qiblah katika swalah iliyopendekezwa wakati wa Takbiyrat-ul-Ihraam kisha baada ya hapo akaelekea ule upande kifaa kinakwenda, basi kufanya hivo ndio bora zaidi. Kwa sababu hayo yamethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika baadhi ya Hadiyth.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/408)
  • Imechapishwa: 15/11/2021