02. Ulazima wa swalah ya mkusanyiko ndani ya Sunnah

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimetamani niamrishe kuswaliwe ambapo ikasimamishwa kisha nikamwamrisha mtu awaswalishe watu halafu nikaondoka na kikosi cha wanamme walio na vifurushi vya kuni kuwaendea watu ambao hawashuhudii swalah nikazichoma nyumba zao kwa moto.”[1]

Katika “Musnad” ya Imaam Ahmad kumepokelewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Kama sio majumba kuwa na wanawake na watoto basi ningezichoma.”[2]

Katika “Swahiyh” ya Muslim kutoka kwa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´an) aliyesema:

“Tulikuwa tukiona hakuna anayeiacha [swalah ya mkusanyiko] isipokuwa ni mnafiki ambaye unatambulika unafiki wake au mgonjwa. Mtu alikuwa akibebwa kati ya watu wawili mpaka anasimamishwa katika safu.”[3]

Amesema tena:

“Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametufunza njia za uongofu. Hakika miongoni mwa njia za uongofu ni kuswali katika msikiti ambao kunaadhiniwa ndani yake.”

Vilevile imepokelewa kutoka kwake:

“Anayetaka kukutana na Allaah kesho hali ya kuwa muislamu basi azihifadhi swalah hizi pindi zinaponadiwa. Hakika Allaah amemuwekea Nabii Wake njia za uongofu – nazo ni njia za uongofu. Endapo mtaswali majumbani mwenu kama anavoswali nyumbani kwake huyu anayebaki nyuma basi mtakuwa mmeiacha njia ya Mtume wenu. Mkiacha njia ya Mtume wenu basi mtapotea. Hakuna mtu anayejitwahirisha akaweka vizuri twahara yake kisha akaenda msikitini miongoni mwa misikiti hii isipokuwa Allaah atamwandikia jema moja, atamuinua ngazi na kumfutia kosa moja kwa kila hatua anayopiga. Tulikuwa tukiona hakuna anayeiacha [swalah ya mkusanyiko] isipokuwa ni mnafiki ambaye unatambulika unafiki wake au mgonjwa. Mtu alikuwa akibebwa kati ya watu wawili mpaka anasimamishwa katika safu.”[4]

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim pia amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema: “Bwana mmoja kipofu alisema: “Ee Mtume wa Allaah! Sina kiongozi wa kuniongoza msikitini. Je, ninayo ruhusa ya kuswali nyumbani kwangu?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Je, wasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Basi imewajibika.”[5]

Vilevile imesihi kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Atakayesikia wito na asiutikie basi hana swalah isipokuwa kutokana na udhuru.”[6]

 Kukasemwa: “Ee Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu anhumaa)! Udhuru ni upi?” Akasema: “Khofu au maradhi.”

Hadiyth zinazofahamisha kuwa ni lazima kuswali katika mkusanyiko na kwamba ni lazima kuswali katika nyumba za Allaah ni nyingi sana.

[1] al-Bukhaariy (6683) na Muslim (1041) na tamko ni lake.

[2] Muslim ameipokea katika ”Baaqiy Musnad-ul-Mukaththiriyna” (8441).

[3] Muslim (1045).

[4] Muslim (1046).

[5] Muslim (653) na an-Nasaa´iy (850).

[6] Abu Daawuud (551) na Ibn Maajah (793).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 13-15
  • Imechapishwa: 15/11/2021