01. Ulazima wa swalah ya mkusanyiko ndani ya Qur-aan

Nimefikiwa na khabari kwamba waislamu wengi wanazembea kuswali swalah katika mkusanyiko na wanajengea hoja kwa kitendo cha baadhi ya wanazuoni kuchukulia wepesi jambo hilo. Kwa hivyo ikanilazimu kubainisha ukubwa na ukhatari wa jambo hili. Hapana shaka yoyote kwamba kitendo hicho ni uovu mkubwa na khatari kubwa. Ni lazima kwa wanazuoni kuzindua jambo hilo na kulionya kwa sababu ni maovu ya wazi yasiyofaa kunyamaziwa.

Inatambulika kwamba haitakikani kwa muislamu kuchukulia wepesi jambo ambalo Allaah ametukuza shani yake katika Kitabu Chake kitukufu. Aidha Mtume Wake pia mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatukuza jambo lake.

Allaah (Subhaanah) ndani ya Kitabu Chake kitukufu ametaja swalah kwa wingi na akatukuza shani yake. Ameamrisha kuihifadhi na kuitekeleza katika mkusanyiko. Amekhabarisha kwamba kuipuuza na kuichukulia wepesi ni miongoni mwa sifa za wanafiki. Amesema (Ta´ala) katika Kitabu Chake kinachobainisha:

حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ

”Shikamaneni na swalah na khaswakhaswa swalah ya katikati na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu.”[1]

Ni vipi watu watajua namna mja anavoihifadhi na kuitukuza ilihali ameacha kuiswali pamoja na ndugu zake na akapuuza jambo lake? Amesema (Ta´ala):

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَارْكَعُوا مَعَ الرَّاكِعِينَ

“Simamisheni swalah na toeni zakaah na rukuuni pamoja na wanaorukuu.”[2]

Aayah hii tukufu ni dalili juu ya ulazima wa kuswali kwa mkusanyiko na kushirikiana na waswaliji katika swalah yao. Ikiwa malengo ni kule kuitekeleza peke yake hakudhihiri mafungamano ya wazi mwisho mwa Aayah pale aliposema (Subhaanah):

وَارْكَعُوا مَعَ الرَّاكِعِينَ

“… na rukuuni pamoja na wanaorukuu.”

Kwa vile ameamrisha kuitekeleza mwanzoni mwa Aayah:

وَإِذَا كُنتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ الصَّلَاةَ فَلْتَقُمْ طَائِفَةٌ مِّنْهُم مَّعَكَ وَلْيَأْخُذُوا أَسْلِحَتَهُمْ

“Utapokuwa upo kati yao ukawaswalisha, basi lisimame kundi miongoni mwao pamoja nawe na wabebe silaha zao.”[3]

Akawajibisha (Subhaanah) kutekeleza swalah kwa mkusanyiko katika hali ya vita na khofu kali. Tusemeje katika hali ya amani? Kama angelikuwa yeyote ambaye anaruhusiwa kuacha kuswali kwa mkusanyiko basi wapanga safu kwa ajili ya maadui na wanaotishiwa kushambuliwa wangelikuwa na haki zaidi ya kuruhusiwa kuacha kuswali kwa mkusanyiko. Wakati mambo hayakuwa hivo basi ikatambulika kuwa kutekeleza swalah kwa mkusanyiko ni miongoni mwa mambo muhimu zaidi ya wajibu na kwamba haijuzu kwa yeyote kuiacha.

[1] 02:238

[2] 02:43

[3] 04:102

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 11-13
  • Imechapishwa: 15/11/2021