Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

52- Allaah ametakasika kutokamana na mipaka, miisho, viungo vya mwili na zana. Hazungukwi na pande sita kama ilivyo kwa viumbe vyote[1].

[1] Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah):

“Kuna ujumla katika maneno haya na yanaweza kutumiwa na wale watu wenye kupindisha na kupotosha majina na sifa za Allaah. Hata hivyo hawana hoja yoyote, kwa sababu makusudio yake (Rahimahu Allaah) ni kumtakasa Muumba kutokamana na kufanan na viumbe. Pamoja na kwamba amekuja na ibara ambazo ni za jumla ambazo zinahitaji kupambanuliwa ili kuondoke mambo ya utata.

Makusudio ya mipaka ni ile inayotambulika kwa mwanadamu. Hakuna yeyote anayejua mipaka Yake isipokuwa Yeye (Subhaanah). Kwani viumbe hawamzunguki kiujuzi. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا

“Anajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na wala hawawezi kumzunguka Yeye wote kiujuzi.” (20:110)

Salaf waliozungumzia kuhusu kikomo katika kulingana na nyenginezo walikusudia mpaka unaotambulika na Allaah (Subhaanah) na si viumbe.

Kuhusu ibara miisho, viungo vya mwili na zana, makusudio yake (Rahimahu Allaah) ni kumtakasa katika hekima Yake na sifa Zake za kidhati (kama uso, mkono na mguu) kufanana na viumbe. Yeye (Subnaanah) ni Mwenye kusifika kwa sifa hizo, lakini sifa Zake si kama sifa za viumbe. Hakuna yeyote anayejua namna zilivyo isipokuwa Yeye (Subhaanah).

Ahl-ul-Bid´ah wanatumia matamshi kama haya kwa ajili ya kukanusha sifa za Allaah. Hawatumii matamshi yaliyotumiwa na Allaah na zile sifa ambazo Amejithibitishia nazo Mwenyewe ili wasije kufedheheka na kukaripiwa na watu wa haki. Mtunzi wa kitabu at-Twahaawiy hakuwa na makusudio kama walionayo wao kwa sababu yeye ni katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambaye anazithibitisha sifa za Allaah. Maneno yake katika kijitabu hiki yanajifasiri yenyewe kwa yenyewe. Yale yasiyokuwa wazi yanatakiwa kufasiriwa kwa yale yaliyo wazi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haashiyah ´alaa al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 33-34
  • Imechapishwa: 15/11/2021