Swali: Je, mtu analazimika kusema “Allaahu Akbar” katika Sujuud ya kisomo ndani ya swalah na nje yake? Je, ni lazima kutoa salamu nje yake?

Jibu: Sujuud ya kisomo ni kama Sujuud ya swalah. Akisujudu katika swalah anatakiwa kuleta Takbiyr na akiinuka pia anatakiwa kuleta Takbiyr akiwa ndani ya swalah. Dalili ya hayo ni yale yaliyothibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba ndani ya swalah alikuwa anasema “Allaahu Akbar” kila anapoteremka na anapoinuka. Akisujudu analeta Takbiyr na akiinuka analeta Takbiyr. Hivi ndivo walivyomuelezea Maswahabah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ya Abu Hurayrah na wengineo.

Kuhusu akisujudu kwa ajili ya kisomo nje ya swalah basi hakuna kilichopokelewa isipokuwa kuleta Takbiyr mwanzoni mwake. Hichi ndicho kinachotambulika. Ameyapokea Abu Daawuud na al-Haakim. Kuhusu anapoinuka nje ya swalah hakukupokelewa juu yake Takbiyr wala Tasliym.

Baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa atasema “Allaahu Akbar” wakati wa kuinuka na kuleta Tasliym pia. Lakini hakukupokelewa chochote juu ya hilo. Kwa hivyo hakukusuniwa kwake isipokuwa kuleta Takbiyr ya kwanza pindi anaposujudu akiwa yuko nje ya swalah.

Kilichosuniwa katika sijda ya kisomo ni yeye kusema yale anayoyasema katika Sujuud ya swalah ambayo ni Tasbiyh na du´aa. Wakati wa kuinuka hakuna Tashahhud wala kuleta Takbiyr. Wala asilete Tasliym kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Kwani hayo hayakupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/410)
  • Imechapishwa: 15/11/2021