Shaykh Swaalih Aalish-Shaykh kuhusu kuwatukana Maswahabah

Kuwatukana Maswahabah kumegawanyika aina zifuatazo:

Ya kwanza: Mwenye kuwatukana wote au akahukumu wengi wao ukafiri au kwamba ni wenye kuritadi – isipokuwa wachache – hii ni kufuru. Huyu amerudisha ushuhuda wa Allaah (´Azza wa Jall) pale aliposema:

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ

“Kwa hakika Allaah amewaradhi waumini walipofungamana nawe ahadi ya utiifu chini ya mti.” (48:18)

Imethibiti kwamba wale waliotoa kiapo cha usikivu na utiifu walikuwa ni Maswahabah elfu moja na mia nne na katika baadhi ya mapokezi imekuja kwamba walikuwa elfu moja na mia tano .

Ya pili: Mtu akatukana baadhi yao. Hili linahitajia ufafanuzi:

1- Akiwatukana baadhi yao kwa kufahamu kimakosa kwa njia ya kwamba akawa ni mwenye kuamini kuwa walikosea, walizembea na kadhalika, kama wanavyoamini Khawaarij, hii ni dhambi kubwa na haimfanyi mtu akatoka katika Uislamu.

2- Akiwatukana baadhi yao kwa ajili ya chuki na kuwa na vifundo juu yao ni kufuru na linamtoa mtu katika Uislamu. Wanachuoni wamesema kuwa hilo ni kwa sababu Allaah (´Azza wa Jall) amesema alipokuwa akiwasifu Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ

“… ili wawakasirishe makafiri.” (48:29)

Yule ambaye ana chukijuu ya Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi anatakiwa kusifiwa kama ambavyo Allaah (Ta´ala) alivyomsifu ya kwamba ni katika makafiri.

Kuhusiana na wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hukumu ya kuwatukana ni kama hukumu ya kuwatukana Maswahabah.

Ama kuwachafua wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au mmoja wao – ni mamoja awe ni ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) au wengineo – na kusema kwamba hakuwa mwanamke aliyetulia, ni kumkufuru Allaah. Yule mwenye kumchafua mmoja katika wakeze Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba hakuwa mwanamke mwenye kutulia ni kafiri. Kwa sababu atakuwa amerudisha maneno ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) na yale aliyomhukumia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalish-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 145-146
  • Imechapishwa: 27/08/2020