Shaykh na imamu – majina yanayotumika vibaya hii leo

Swali: Je, ni sahihi kumwita “Shaykh” kila mmoja khaswa kwa kuzingatia kwamba jina hilo limekuwa lenye kuenea sana?

Jibu: Neno “Shaykh” kwa mujibu wa kiarabu halitumiwi isipokuwa kwa mtu mkubwa; ima ni mkubwa kiumri au mkubwa kingazi kwa elimu, mali yake au kadhalika. Halitumiwi kwa mtu mdogo. Lakini kama ulivosema, hivi sasa neno hilo limekuwa ni lenye kuenea mpaka wajinga au watu wasiojua kitu wamekuwa wakiitwa nalo. Naona ni kitu kisichostahiki. Kwa sababu ukimwita “Shaykh” mtu ambaye ni mjinga watu wataghurika naye na watadhani kuwa anayo elimu. Matokeo yake warejee kwake wakati wa fatwa, jambo ambalo litapelekea katika madhara makubwa.

Kwa masikitiko makubwa watu wengi hawajali kujibu wanapoulizwa maswali, ijapo ni pasi na elimu. Kwa sababu wanaona ni kujipunguza wao wenyewe wakisema kuwa hawajui swali hilo. Ukweli wa mambo ni kwamba mtu akisema kuwa hajui juu ya kile asichokijua, bais hiyo inakuwa ni ukamilifu kwake. Lakini kimsingi ni kwamba watu wanapenda waonekane.

Kwa hivyo naona kuwa neno “Shaykh” lisitumike isipokuwa kwa yule ambaye analistahiki ima kutokana na umri wake, utukufu wake au ngazi alionayo kwa watu wake au kutokana na elimu yake.

Ni kama ambavo hii leo watu wanatumia neno “maimamu” kwa wanachuoni wote. Wanamwita “imamu” ingawa mwanachuoni huyu ni miongoni mwa wale wanaofuata kichwa kibubusa. Hiki pia ni kitu kisichotakiwa. Neno “imamu” halitakiwi kutumiwa isipokuwa kwa yule mwenye kulistahiki. Aidha awe na wafuasi na maoni yake yawe ni yenye kuzingatiwa kati ya waislamu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (117 B)
  • Imechapishwa: 19/05/2021