Maudhi ya mlinganizi yasiyoepukwa

Swali: Nimemnasihi bwana mmoja ambaye anapenda muziki na nikampa kaseti zenye manufa. Kaseti za muziki nilizifuta na kuweka mambo yenye manufaa. Baada ya hapo akarudi kwenye muziki kwa mara nyingine na akaanza kunitukana na kunilaani. Hata hivyo nikamnasihi kwa mara nyingine. Ni ipi hukumu?

Jibu: Nakupa bishara ya kheri kwa kupata maudhi kwa kulingania kwa Allaah. Ambaye analingania kwa Allaah na akaudhiwa kwa ajili ya Allaah na akasubiri, basi ana fungu katika thawabu za walinganizi. Aidha anakuwa ni mwenye kuwaigiliza Mitume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ فَصَبَرُوا عَلَىٰ مَا كُذِّبُوا وَأُوذُوا حَتَّىٰ أَتَاهُمْ نَصْرُنَا

“Kwa hakika walikadhibishwa Mitume kabla yako wakasubiri juu ya yale waliyokadhibishwa na wakaudhiwa mpaka ilipowafikia nusura Yetu; na hakuna abadilishaye maneno ya Allaah. Tayari zimekwishakujia khabari za Mitume.”[1]

Wewe fanya subira juu ya maneno yake. Akikulaani basi wewe fanya subira. Akikulaani na wewe si mwenye kustahiki laana hio, basi laana inamrejelea yeye mwenyewe. Akikutusi basi anakuwa amekupa matendo yake mema. Kwa hivyo fanya subira, tarajia malipo kutoka kwa Allaah na mwombee kwa Allaah uongofu. Endelea kumlingania kwa Allaah yeye na wengine na subiri kwa yale yote yanayokufika. Hukusikia namna ambavo Luqmaan alimsihi mwanae:

يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَى مَا أَصَابَكَ

“Ewe mwanangu! Simamisha swalah, na amrisha mema, na kataza maovu na subiri kwa yanayokupata.”[2]

Mlinganizi ambaye analingania kwa Allaah kwa kuamrisha mema na kukataza maovu anapaswa kufikwa na maudhi. Kwa ajili hiyo anatakiwa kufanya subira na kutaraji malipo kutoka kwa Allaah na Allaah atamlipa thawabu kwa kule kuamrisha, kukataza na subira ya maudhi anayopata.

[1] 06:34

[2] 31:17

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (30 B)
  • Imechapishwa: 19/05/2021