“Salafiyyah yetu ni yenye nguvu kuliko Salafiyyah ya al-Albaaniy”      

Shaykh Muhammad bin Haadiy al-Madkhaliy (Hafidhwahu Allaah) ndio amesoma swali:

“Nimekusikia unasema: “Salafiyyah yetu ni yenye nguvu kuliko Salafiyyah ya al-Albaaniy.” Anataka kuwekewa wazi maneno haya.

Jibu: Nimeshajibu swali hili idadi ya mara zisizojulikana na hili ni kama kauli inayosema: “Shaykh al-Albaaniy anamponda Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab.” Mnasema nini juu ya madai haya? Hamna jibu? Mimi nimelijibu na kuweka wazi uongo wao. Watu hawa ambao wanakariri swali hili ni waongo. Hawana himaya yoyote kwa Shaykh al-Albaaniy, si kwa karibu wala kwa mbali. Hawakubaliani na yeye wala mfumo wake, bali wanakariri hili ili kueneza fitina. Haya ndio makusudio yao. Mimi namuheshimu al-Albaaniy na sidhani kama kuna yeyote ambaye anamuheshimu zaidi kuliko mimi ninavyomuheshimu. Nimemtetea – himdi zote ni Zake Allaah – mara nyingi sana. Neno hili lenyewe nimelifanya kwenye kanda ambayo nilikuwa namtetea Shaykh al-Albaaniy. Je, ina maana ya dharau wakati Imaam ash-Shaafi´iy alipomwambia Imaam Ahmad bin Hanbal na wenzake:

“Nyinyi ni wajuzi zaidi ya Hadiyth kuliko mimi. Hivyo nielezeni Hadiyth yoyote ambayo ni Swahiyh, sawa ikiwa ni ya kutoka al-Kuufah, al-Baswrah, ash-Shaam au Misri.”?

Ahmad alikuwa ni mjuzi zaidi katika Hadiyth kuliko yeye na elimu ya wanaume. Je, hii nidharau kwa ash-Shaafi´iy? Mifano ya maana kama hiyo ni mingi. Shaykh al-Albaaniy alisema kuhusu Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab:

“Ni Shaykh-ul-Islaam wa pili.”

Je, mwenye kusema maneno haya kwa Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab anamdharau? Nilimtetea Shaykh al-Albaaniy tena na tena na tena. Nikabainisha nafasi yake, Jihaad yake, elimu yake, kuilinda kwake Sunnah na kupiga vita Bid´ah, kueneza Sunnah na kadhalika. Walisema kwanza ya kwamba sisi hatukujua Salafiyyah isipokuwa al-Albaaniy alipokuja kutufunza nayo, na kwamba sisi ni kundi la al-Albaaniy. Tukajadiliana naye katika zile siku za mwanzo wakati alipokuja katika chuo kikuu [cha Kiislamu al-Madiynah] kutufunza. Naonelea kuwa Salafiyyah yetu ni yenye nguvu kuliko ya kwake. Shaykh al-Albaaniy anaoenelea kuwa sisi ni wenye misimamo mikali, wakati na sisi tunaonelea kuwa ni mlaini. Hivyo ndivyo nilivyosema. Huku sio kumdharau. Je, ina maana ya kwamba tumemdharau? Kamwe hatufanyi hivyo kwake.

Kwa hali yoyote, ´Aqiydah yetu na mfumo wetu ni mmoja na ni ileile. Shaykh Ibn Baaz, Shaykh Ibn ´Uthaymiyn, Shaykh al-Albaaniy, Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab na Ibn Taymiyyah wote wako katika ´Aqiydah na mfumo mmoja.

Malengo ya swali kama hili ni kutaka kuwafanya Salafiyyuun wazozane wao kwa wao. Lau Shaykh al-Albaaniy angelifikiwa na hili, asingelichukulia vibaya[1]. Hili limewafikia wanafunzi wake na hawakulichukulia kwa ubaya. Hawa ambao wanazozana juu yalo mimi naamini kuwa ni maadui wa al-Albaaniy, mfumo wake, na wanachotaka kwa hilo ni kueneza fitina.

Mimi simtuhumu muulizaji huyu ambaye ameniuliza hivi sasa. Pengine amepata mawazo kutoka kwa watu hawa waharibifu na hivyo ndio akawa ameniuliza swali hili.

[1] Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema katika kanda “ash-Shiddah ´inda as-Salafiyyiyn”:

“Ukiuliza kuhusu hali yangu, nitasema kuwa mimi ni mlaini.”

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kutoka katika kanda “Salafiyyatunaa aqwaa min Salafiyyatiy al-Albaaniy – ash-Shubhah war-Radd ´alayhaa”
  • Imechapishwa: 20/07/2020