Swali: Katika mazingira haya yaliyojaa makundi wamekuwa wengi wanaojinasibisha na Salafiyyah. Bali wamekuwa wengi wanaojidai wenyewe Salafiyyah na kuwakataza wengine kuingia ndani ya Salafiyyah. Kuna kidhibiti kipi cha Salafiyyah?

Jibu: Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ

“Wale waliotangulia wa mwanzo [katika Uislamu] miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema.”[1]

Salafiyyah imejengeka katika mfumo wa wale waliotangulia awali, katika wale ambao walihajiri na wakasaidia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego yenu.”

Salafiy wa kikweli ni yule anayewafuata Salaf kwa wema pasi na kuchupa mipaka wala kuzembea. Anakuwa kati na kati kwa mujibu wa mfumo wa Salaf. Sio kila ambaye anajiita kuwa ni ”Salafiy” anakuwa hivyo. Hawi Salafiy ikiwa hawafuati kwa wema. Kuwafuata kwa wema maana yake ni kwa ustadi. Hawezi kuwafuata Salaf kwa wema isipokuwa pale atapojifunza ´Aqiydah yao sahihi na mfumo wao ili aweze kuufuata kwa njia sahihi. Salafiyyah sio madai peke yake yaliyoandamana na ujinga. Hili linahitaji elimu na utambuzi ili tuweze kuwafuata kwa wema.

[1] 09:100

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://alfawzan.af.org.sa/ar/node/5409 Tarehe: 1427-11-02/2006-11-22
  • Imechapishwa: 13/11/2022