Imethibiti kwa wanachuoni wengi wa Taabi´uun wakikataza kukaa na Ahl-ul-Bid´ah wal-Ahwaa´. Hilo si kwa sababu ya jengine isipokuwa ni kwa kukhofia mzushi huyo asije akamuathiri mwenye kukaa naye. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amehimiza juu ya kukaa na mtu mwema na akatahadharisha na kukaa na mtu muovu. Amepigia mfano wa kikao cha mtu mzuri ni kama muuza manukato na kikao cha mtu muovu ni kama muhunzi. Kukaa na mtu mwema ni kama muuza manukato; ima ukanunua kutoka kwake, akakupa au na wewe ukanukia vizuri. Kuhusiana na kikao cha mtu muovu ni kama muhunzi; ima akaiunguza nguo yako au na wewe ukapatwa na harufu mbaya.

Vivyo hivyo inakuwa kwa mzushi; ima akaiingiza kwenye moyo wako Bid´ah kwa kukupendezea nayo au akaugonjwesha moyo wako kutokamana na yale matendo utayoyashuhudia kwake na maneno utayoyasikia kutoka kwake katika mambo ambayo yanaenda kinyume na Shari´ah. Kwa ajili hii al-Hasan amesema:

“Usikae na mtu anayefuata matamanio akaingiza kwenye moyo wako yatayofanya umfuate hatimaye ukaja kuangamia au ukaenda kinyume naye moyo wako ukaingiwa na maradhi.”

Amesema tena:

“Usikae na mtu anayefuata matamanio akaufanya moyo wako kuwa na maradhi.”

Abu Qilaabah amesema:

“Usikae na Ahl-ul-Ahwaa´ na wala usijadiliane nao. Mimi nachelea wasije kukuingizeni katika upotevu wao na wakakutatizeni mambo mliyokuwa mkiyajua.”

Ayyuub amesema kuhusu Abu Qilaabah:

“Alikuwa ni katika wanachuoni wa Fiqh na mwenye akili.”

Amesema tena:

“Ahl-ul-Ahwaa´ ndio wapotevu. Sioni mafikio yao mengine zaidi ya Motoni.”

Amesema vilevile:

“Hakuna mtu aliyezusha Bid´ah isipokuwa alihalalisha pia kuua.”[1]

Ayyuub as-Sikhtiyaaniy alikuwa akisema:

“Mtu wa Bid´ah kadri na jinsi anavyofanya bidii ndivyo kunavyozidi kumuweka mbali na Allaah. Alikuwa akiwaita Ahl-ul-Bid´ah ´Khawaarij`. Vilevile alikuwa akisema: “Khawaarij wametofautiana kwa majina na wamekusanyika juu ya kuua.”[2]

Yahyaa bin Kathiyr amesema:

“Ukikutana na mtu wa Bid´ah njiani basi badili upite njia nyingine.”

[1] “al-I´tiswaam” ya as-Shaatwibiy (01/83).

[2] “al-I´tiswaam” ya as-Shaatwibiy (01/73).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Bid´ah – Dhwawaabitwuhaa wa atharuhaa as-Sayyiu´ fiyl-Ummah, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 27/08/2020