Alikuwa akiitwa Sa´iyd bin Zayd bin Nufayl bin ´Abdil-´Uzzaa bin Rayaah bin Qurtw bin Razaah bin ´Adiyy bin Ka´b bin Lu-ayy bin Ghaalib, Abul-A´war al-Qurashiy al-´Adawiy.

Ni mmoja katika wale kumi walioahidiwa Pepo na ni miongoni mwa wale waliotangulia wa mwanzo ambao walioshuhudia vita vya Badr. Ni mmoja katika wale ambao Allaah amewaridhia nao wakamridhia.

Alishuhudia vita pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alishuhudia kuizingira Dameski na kuifungua. Baada ya hapo Abu ´Ubaydah akamtawalisha Dameski. Kwa hivyo yeye ndiye naibu wa kwanza Dameski kutoka katika Ummah huu.

Mke wake alikuwa binamu yake Faatwimah, dada yake na ´Umar bin al-Khattwaab.

Amepokea Hadiyth chache. Miongoni mwa hizo ziko mbili kwa al-Bukhaariy na Muslim. al-Bukhaariy amepwekeka na moja.

Miongoni mwa waliopokea kutoka kwake ni Ibn ´Umar, Abu Twufayl, ´Amr bin Haarith na wengineo.

Sa´iyd bin Zayd amesema:

“´Umar alinifungamanisha mimi na dada yake kwa ajili ya Uislamu.”[1]

Hishaam amepokea kutoka kwa baba yake kwamba Arwaa bint Uways alidai kwamba Sa´iyd bin Zayd amechukua kipande cha ardhi yake na akapeleka mashtaka kwa Marwaan. Ndipo Sa´iyd akasema: “Hivi kweli mimi nitachukua kipande cha ardhi yake baada ya kuwa nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Yule ambaye atachukua chochote kutoka katika ardhi, basi atabebeshwa shingoni mwake adidimie kwenda mpaka katika ardhi ya saba.”?[2]

Ndipo Marwaan akasema:

“Sihitajii ushahidi mwingine baada ya haya.”

Sa´iyd akasema:

“Ee Allaah! Akiwa ni mwongo basi yapofoe macho yake na muue katika ardhi yake.”

Hakufariki mpaka alipofoka. Siku moja wakati alipokuwa akitembea juu ya ardhi yake alitumbukia kwenye shimo akafa.

Sa´iyd bin Zayd amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´aalyhi wa sallam) alikuwa juu ya Hiraa´ na akauambia: ”Tulizana, ee Hiraa´! Hakuna aliye juu yako zaidi ya Nabii, mkweli au shahidi.” Waliokuweko juu ni Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy, Twalhah, az-Zubayr, Sa´d, ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf na Sa´iyd bin Zayd.”[3]

Naafiy´ amesema:

“Sa´iyd bin Zayd alikufa baada ya kuwa na matatizo ya kuendesha. Ndipo akasema mama yake kumwambia ´Abdullaah bin ´Umar: “Unampaka miski?” Akasema: “Ni manukato gani mazuri zaidi kushinda miski?” Ndipo akampa miski.”[4]

´Aaishah bint Sa´d amesema:

“Sa´iyd bin Zayd alikufa ´Aqiyq. Sa´d bin Abiy Waqqaas akamuosha na akamvika sanda na akatoka naye.”[5]

Maalik amesema:

“Sa´iyd bin Zayd na Sa´d bin Abiy Waqqaas wote wawili walifikia´Aqiyq.”

al-Waaqidiy amesema:

“Sa´iyd bin Zayd alikufa mwaka wa 51. Alikufa akiwa na miaka sabini na kitu. Alizikwa al-Madiynah. Sa´d na Ibn ´Umar ndio walioteremka ndani ya kaburi lake.”

Hivo pia ndivo alivosema Abu ´Ubayd, Yahyaa bin Bukayr na Shihaab.

al-Waaqidiy amesema:

“Sa´iyd alikuwa kahawia, mrefu na mwenye nywele.”

[1] al-Bukhaariy (3862).

[2] Muslim (1610).

[3] Ahmad (1/187), Abu Daawuud (4648), at-Tirmidhiy (3758) na Ibn Maajah (134).

[4] Ibn Sa´d (3/1/280).

[5] Ibn Sa´d (3/279).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (1/124-143)
  • Imechapishwa: 11/01/2021