Swali: Ni yapi maoni yako kwa mtu ambaye anachukua ujira mkubwa kwa ajili ya kuwasomea wagonjwa na anatumia hoja ya kusema kwamba ni pesa ya maji, mafuta na asali ambayo anasoma kwayo?

Jibu: Mosi haitakikani kufanya Ruqyah ndio kazi. Haitakikani kuwa ndio chanzo cha chumo lake. Atafute riziki kwa njia nyingine. Awasomee watu kwa njia ya kufanyia wema. Wakimpa kitu haina neno akakipokea. Hata hivyo haifai kwake akafanya hiyo kama kazi na akafungua kliniki ya Ruqyah. Huenda hata hastahiki kufanya Ruqyah. Kuna baadhi ya watu ambao hawastahiki, lakini wanachotaka ni pesa na kuwatia watu mchanga machoni. Watu kama hawa wanatakiwa kukatazwa. Ruqyah ni kitendo cha kuheshimika na kinatakiwa kutendewa kazi tu na wajuzi na wanazuoni walio na ´Aqiydah sahihi. Inatakiwa iwe imejengwa juu ya Qur-aan na du´aa zilizowekwa katika Shari´ah, sio kwa ukhurafi, maneno yasiyofahamika au majina ya mashaytwaan; ni haramu na ni kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Asifanye Ruqyah isipokuwa tu mtu ambaye ana elimu, maarifa na ´Aqiydah sahihi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Tafsiyr-ish-Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (24) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/tafsir-ayat-qrran-19-07-1435-01.mp3
  • Imechapishwa: 20/06/2020