Radd kwa wenye kuona kuwa mwenye kuacha swalah sio kafiri

Swali: Ni ipi Radd kwa mwenye kusema kwamba haikuwa ni jambo lililotangaa kwa Salaf kumtoa katika dini mwenye kuacha swalah?

Jibu: Kurejelewe maneno ya wanazuoni kama vile Ibn-ul-Qayyim katika “as-Swalaah”, katika “al-Mughniy”, “al-Muhallaa” ya Ibn Hazm na mfano wao ambao wametaja makinzano na wakataja dalili za pande zote mbili. Kurejelewe vitabu vya wanazuoni na afaidike. Mengi ambayo wanatumia kama dalili wale wasiooonelea kwamba mwenye kuacha swalah ni kafiri ni Hadiyth za upwekeshaji, ubora wa upwekeshaji na kwamba yule mwenye kukutana na Allaah hali ya kumwabudu Allaah pekee ataingia Peponi na kwamba yule mwenye kukutana Naye akiwa na shirki ataingia Motoni. Jawabu ya hayo ni kwamba makusudio ni kwa yule mwenye kukutana Naye hali ya kumwabudu Yeye pekee na sambamba na hilo akasalimika kutokana na vichenguzi vya Uislamu. Yule mwenye kukutana Naye hali ya kumwabudu Yeye pekee na sambamba na hilo akasalimika kutokana na vichenguzi vya Uislamu ndiye ambaye ataingia Peponi. Kuhusu ambaye atakutana na Allaah akiwa na upwekeshaji, hata hivyo yuko na kichenguzi moja wapo cha Uislamu ameharibu upwekeshaji wake. Mifano ya hayo ni mingi; mnasemaje endapo amekutana na Allaah akiwa na upwekeshaji lakini sambamba na hilo anapinga kuwa swalah ni wajibu? Anakufuru au hakufuru? Upwekeshaji wake unabatilika au haubatiliki? Anakufuru au hakufuru akikutana na Allaah akiwa na upwekeshaji lakini sambamba na hilo anasema kuwa zakaah sio wajibu kwa waislamu? Anakufuru au hakufuru akikutana na Allaah akiwa na upwekeshaji lakini sambamba na hilo anasema kuwa kufunga mwezi wa Ramadhaan sio wajibu? Anakufuru au hakufuru akikutana na Allaah akiwa na upwekeshaji lakini sambamba na hilo anasema kuwa hijjah kwa wenye uwezo sio wajibu? Wanazuoni wote wameafikiana kuwa mtu kama huyo ni kafiri na hivyo upwekeshaji wake haumsaidii kitu muda wa kuwa yuko na kichenguzi. Hukumu ni hiyohyo inamuhusu ambaye atakutana na Allaah ilihali haswali. Ni vipi hali ya mwenye kukutana na Allaah akiwa na upwekeshaji lakini sambamba na hilo anasema kuwa Muhammad ni mwongo? Mtu kama huyo ni kafiri kwa mujibu wa wanazuoni wote. Mfano mwingine amekutana na Allaah akiwa na upwekeshaji lakini sambamba na hilo anachezea shere hukumu ya Allaah, kama vile ya Jihaad, swawm au uharamu wa uzinzi, na kuonelea kuwa mambo hayo ni upuuzi. Ni ipi hukumu ya mtu huyo? Ni kafiri. Radd kwao ni nyepesi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/24137/ما-الرد-على-من-انكر-كفر-تارك-الصلاة
  • Imechapishwa: 08/09/2024