Allaah (Ta´ala) amesema:
مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ
“Atakayemtii Mtume basi hakika amemtii Allaah.”[1]
Mwenye kumtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyoamrisha na kukataza, huyu anamtii Allaah (´Azza wa Jall). Aayah inafahamika namna hii. Upande mwingine yule mwenye kumuasi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi amemuasi vilevile Allaah.
Katika Aayah hii kuna dalili juu ya kwamba yale yaliyothibiti katika Sunnah ni kama yaliyothibiti katika Qur-aan. Kwa msemo mwingine ni katika Shari´ah ya Allaah na ni wajibu kushikamana nayo bara bara. Haijuzu kwa yeyote kutofautisha kati ya yaliyothibiti katika Qur-aan na Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alieleza hali ya kuwa ni mwenye kutoa matahadharisho pale aliposema:
“Pengine kukawepo baadhi katika nyinyi mwenye kuketi juu ya kitanda chake. Anapojiwa na kitu kutoka kwangu anasema “Hatujui. [Sisi] tunafuata yale tumeyoyapata katika Kitabu cha Allaah.”[2]
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatahadharisha na kusema huenda kukafika wakati katika zama watu wakasema “Tunafuata tu yaliyoko katika Qur-aan. Kuhusiana na yaliyokuja katika Sunnah sisi hatuyachukui.” Jambo hili limetokea. Kumepatikana katika wakaMungu wenye kusema kuwa hawakubali Sunnah na wao wanakubali Qur-aan tu. Uhakika ni kwamba wamesema uongo. Hawakukubali si Sunnah wala Qur-aan. Kwa sababu Qur-aan inatoa dalili kuonesha uwajibu juu ya kufuata Sunnah na kwamba yaliyokuja katika Sunnah ni kama yaliyokuja katika Qur-aan. Lakini watu hawa wanawapaka mchanga wa machoni wasiokuwa wasomi na kuwaambia Sunnah sio kama Qur-aan yenye kusomwa na haikupokelewa kwa mapokezi mengi kwa waislamu. Hivyo inatia mashaka, inaweze kusahauliwa, kupokewa kimakosa na kadhalika.
[1] 4:80
[2]Abu Daawuud (4605) na at-Tirmidhiy (2663).
- Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/264)
- Imechapishwa: 29/10/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)